Na Pamela Mollel, Arusha
Mkoa wa Arusha umeelezwa kuwa ngome ya amani na utulivu, huku wananchi wake wakiendelea na shughuli za uzalishaji mali kwa ufanisi mkubwa, matokeo ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kauli hiyo imetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Longido, Mhe. Salum Abdalah Kali, wakati akitoa salamu za Mkoa wa Arusha kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, katika ufunguzi wa Mkutano wa Wenyeviti wa Bodi na Watendaji Wakuu wa Taasisi za Umma – CEOs Forum 2025 unaoendelea Agosti 24, 2025 katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa Arusha (AICC).
Amesema Serikali imefanya mageuzi makubwa ya maendeleo kupitia miradi ya kimkakati inayogusa maisha ya wananchi, hususan vijijini.
Aidha Arusha imenufaika kwa kiwango kikubwa ikiwemo kupokea shilingi bilioni 298 kwa ajili ya ujenzi wa uwanja wa mpira wa kimataifa kwa maandalizi ya AFCON 2027, shilingi trilioni 1.6 kwa ujenzi wa kiwanda cha magadi soda Wilaya ya Monduli, shilingi bilioni 236 kwa kujenga stendi ya kisasa Jijini Arusha, shilingi bilioni 20 kwa ukarabati wa barabara za ndani ya Jiji na shilingi bilioni 4 kwa ujenzi wa barabara ya Arusha–Namanga inayounganisha Tanzania na Kenya.
Aidha, amebainisha kuwa kata zote 154 na vijiji 394 vya Mkoa wa Arusha tayari vimeunganishwa na umeme huku 90% ya vitongoji navyo vikifikiwa. Pia, ujenzi wa hospitali ya kisasa yenye upekee wa kuwa na uwanja wa ndege juu ya jengo unaendelea, hatua inayoashiria sura mpya ya huduma za afya na maendeleo ya miundombinu mkoani humo.
Akihitimisha, Mhe. Kali aliwahimiza wajumbe wa mkutano huo kutumia nafasi ya uwepo wao Arusha kufurahia mandhari ya kuvutia, hali ya hewa safi na vivutio vya kipekee vya utalii, ikiwemo mbuga za wanyama chini ya usimamizi wa TANAPA.