Pangani, Tanga
Vikundi vilivyopo kata za Pangani ya zamani, Mwera, Pangani Magharibi pamoja na kata zingine wameshukuru Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia mradi wa RISE kwa mafunzo waliyopatiwa na fursa za kiuchumi kwa kuwapatia elimu ya ujasiriamali.
Mafunzo haya yamehusisha ufafanuzi wa kazi ndogo ndogo za matengenezo ya barabara, elimu ya ujasiriamali, elimu ya namna ya kujisajili na kutumia mfumo wa manunuzi NEST pamoja na elimu kwa vitendo ya matengezo ya barabara.
Akizungumza kwa niaba ya wanavikundi wengine, Bw. Kibwana Athuman amesema “Tunashukuru sana TARURA kwa mafunzo haya yamekuwa na manufaa kwetu sisi kama vikundi. Tumeona fursa nyingi katika kujihusisha kwenye matengenezo ya barabara“
Villevile, Bi Salama Shabani wa kikundi cha Combine ground ameelezea namna mafunzo haya yalivowasaidia kama wanawake “kweli tunashukuru kwa mafunzo haya yametufungua macho sisi wanawake kwenye mambo mengi hasa kutumia mifumo mipya kama NEST”.
Mafunzo hayo yamefanyika kwa vikundi 38 kwa ushirikiano na Shikirika la Kazi Duniani (ILO) pamoja na Mamlaka wa Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).
Mtaalamu kutoka PPRA, Bw. Magnus Steve ametoa elimu ya namna vikundi hivyo vinavyoweza kujisajili na kutumia mfumo wa manunuzi wa NEST kama fursa ya kupata zabuni mbalimbali katika maeneo ya ndani na nje ya makazi yao.