Arusha. Serikali imeyataka mashirika ya Umma kujifunza kutoka kwa sekta binafsi kuhusu namna bora ya kuendesha taasisi na hivyo kuongeza ufanisi wao.
Wito huo ulitolewa Agosti 26, 2025, na Naibu Waziri Mkuu, Mhe. Dk. Doto Biteko wakati wa kufunga Kikao Kazi cha Wenyeviti wa Bodi na Watendaji wakuu wa Taasisi za Umma, jijini Arusha.
Alisema hakuna sababu inayozuia Taasisi za Umma kuweza kujiendesha kwa ufanisi na weledi na hatimaye kupunguza utegemezi kwa Serikali, na badala yake kuwa mstari wa mbele katika kuchangia kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali.
“Sekta binafsi zinafikiri vizuri na wanajilipa mishahara na kulipa kodi serikalini. Lakini baadhi ya mashirika ya umma bado yanaomba fedha za kujiendesha na mishahara kutoka serikalini kila mwaka,” alisema Dk. Biteko ambaye pia ni Waziri wa Nishati.
Aliongeza: “Ajabu ni kwamba watu wachache katika sekta binafsi wanauwezo wa kuendesha taasisi kwa ufanisi na hivyo kumudu kulipa watumishi wo mishahara.”
Alisema ni katika muktadha huo anaona haja ya Taasisi za Umma kujifunza mbinu ambazo sekta binafsi wanatumia.
“Wakuu wa Taasisi za Umma mnapaswa kuziba mianya ya upotevu wa mapato. Fanyeni kazi ya kusimamia mashirika yenu ili mkawe mafundi wa kurekebisha taasisi zenu na kufikiri tofauti huku mkizingatia ubunifu kama zilivyo sekta binafsi.”
Aidha, Dk. Biteko alibainisha kuwa yapo mageuzi yaliyofanyika kwa mashirika ya umma na kuleta matokeo makubwa kwa Taifa.
“Mageuzi tunayoyasimamia na tunayoyatekeleza katika Mashirika na Taasisi za Umma siyo maneno kwenye makaratasi pekee, bali yameanza kuleta matokeo yanayoonekana kwa Taifa letu.”alisema, akiyataka mashirika mengine pia kuongeza ufanisi.
Mh. Dkt. Biteko pia aliwataka Wenyeviti na Wakuu wa Taasisi za Umma kufanya kazi kwa upendo na kutegemeana ili kuepuka migogoro isiyo na tija.
“Sitaki kusikia Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu mnavutana,” alisisitiza.
Dkt. Biteko aliwataka Wenyeviti na Wakuu wa Taasisi za Umma kuwa mabalozi wa amani kwa taasisi na mashirika wanayosimamia katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba 29, 2025.
“Ni matamanio yetu kama nchi kuwa na uchaguzi wa amani kwani tukiwa na amani, Mashirika yetu ya Umma yatakuwa kwenye nafasi ya kufanya vizuri.” Alisisitiza.
Naye Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais – Mipango na Uwekezaji, Mhe. Stanslaus Nyongo, aliwapa changamoto wenyeviti na wakuu wa Taasisi za Umma kuhakikisha wanaiwezesha Serikali kutekeleza Dira 2050.
“Serikali ina mpango wa kuwa na Uchumi wa Kati wa Juu ifikapo mwaka 2050, huku pato la Taifa likifikia $1 trilioni, ikilinganishwa na $85 bilioni za sasa. Kwahiyo tuna kazi kubwa ya kufanya na tunahitaji utayari wa hali ya juu,” alisema.
Aliongeza: “Hii sio kazi ndogo, tuna kazi kubwa ya kufanya na naamini tukiimarisha mashirika yetu ya Umma tutaweza kufikia adhma hiyo,” alisema Mhe. Nyongo.
Aliongeza kuwa lengo la wizara ni kuhakikisha mashirika na taasisi za umma yanachangia kikamilifu katika uchumi wa taifa letu, ikiwemo Dira 2050.
Kwa upande wake Msajili wa Hazina Bw. Nehemiah Mchechu alisema mageuzi yanayofanyika katika mashirika ya umma tayari yameanza kuazaa matunda.
“Katika awamu ya kwanza mashirika makubwa yakiwemo STAMICO, TANESCO, na TPDC yameweza kuondokana na utegemezi wa ruzuku ya Serikali katika uendeshaji na mishahara,” alisema.
Alieleza kuwa Ofisi inaendelea na uchambuzi utakaowezesha idadi ya Mashirika yanayojitoa katika utegemezi wa Serikali kuongezeka kufikia mwishoni mwa mwaka ujao wa fedha.
“Kujitoa katika utegemezi kunawezesha fedha hizo kutumika katika kuendeleza miradi mikubwa ya maendeleo,” alihitimisha.