
Dar es Salaam, Agosti 26, 2025 – Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa imebatilisha uteuzi wa aliyekuwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina, kuwa mgombea urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama cha ACT-Wazalendo, ikisema uteuzi huo haukufuata taratibu za chama.
Uamuzi huo umetolewa baada ya Msajili kuwaita viongozi wa chama hicho na kusikiliza malalamiko yaliyowasilishwa na Monalisa Ndala, Katibu Mwenezi wa ACT-Wazalendo Mkoa wa Dar es Salaam, ambaye alipinga hatua ya kumpitisha Mpina akidai kanuni na taratibu za chama zilivunjwa.
Tukio hili linakuja siku moja kabla ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) kufanya uteuzi rasmi wa wagombea urais, ubunge na udiwani watakaoshiriki Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Kwa mujibu wa Kanuni za Uchaguzi, hatua inayofuata baada ya uteuzi ni kuweka pingamizi dhidi ya mgombea. Pingamizi linaweza kuwasilishwa na mgombea mwingine, Msajili wa Vyama au Mwanasheria Mkuu wa Serikali. Tarehe ya mwisho ya pingamizi ni Agosti 28 saa 10:00 jioni, isipokuwa pingamizi kutoka kwa Msajili wa Vyama, ambalo linaweza kuwasilishwa ndani ya siku 14 baada ya siku ya uteuzi.
Mpina pamoja na mgombea mwenza wake, Fatma Fereji, tayari walikuwa wamechukua fomu za kuwania urais kupitia INEC na walitarajia kesho, Agosti 27 kuzirejesha kwa ajili ya hatua ya uteuzi.
Wawili hao pia walikuwa wameshakamilisha zoezi la kukusanya wadhamini zaidi ya 200 katika kila mkoa, kwenye mikoa isiyopungua kumi, ikiwemo miwili kutoka Zanzibar, kama sharti la kisheria kwa wagombea wa urais.
Hatua ya Msajili inatarajiwa kuchochea mjadala mpya ndani ya ACT-Wazalendo na katika uwanja mpana wa siasa, hasa ikizingatiwa kuwa uteuzi wa Mpina ulikuwa tayari umeshaibua maoni tofauti miongoni mwa wanachama na wadau wa siasa nchini.