Mtendaji Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta akizungumza na waandishi wa habari jijini Arusha.
Meneja wa TANROADS mkoa wa Arusha , Mhandisi Reginald Massawe akizungumzia kuhusu miradi mbalimbali mkoani Arusha.
…………..
Happy Lazaro, Arusha
MTENDAJI Mkuu wa TANROADS, Mhandisi Mohamed Besta ametoa wito kwa wananchi kuzitumia barabara kwa uangalifu mkubwa hasa kwa wale wenye makampuni ya usafirishaji na kuacha kuzidisha uzito wa magari kupita kiasi ,tushirikiane na serikali kutunza miundombinu ambayo inajengwa kwa gharama kubwa.
Ameyasema hayo jijini Arusha wakati akizungumza katika Tamasha la Samia Connect lililofanyika kwa siku tatu jijini Arusha lenye lengo la kuwapatia wananchi mbalimbali huduma za kijamii.
Mhandisi Besta amesema kuwa, kwa wananchi wa kawaida ambao ni watumiaji wa barabara kwa maana ya kupata usafiri watunze dhamani za barabara kama.zile ambazo zinaonyesha usalama barabarani wasizingoe wakaenda kuzitumia kwa matumizi mengine.
“Nawaomba sana wananchi wa mkoa wa Arusha na Tanzania kuwa waendelee kushirikiana kuhakikisha kuwa barabara zetu zinaendelea kudumu na ziendelee kutusaidia katika kujiendeleza kiuchumi na hivyo kuleta maendeleo katika nchi yetu.”amesema.
Amesema kuwa , TANROADS tuna ushiriki wa hali ya juu katika tamasha hilo ambapo dhamira ni kuonyesha jinsi miundombinu ya barabara na madaraja katika mkoa wa Arusha na Tanzania kwa ujumla inavyotekelezwa na serikali ya Dokta Samia Suluhu Hassan.
Amesema kuwa ,ni moja kati ya sekta muhimu sana ambayo wananchi wangependa kujua nini kinaendelea katika nchi yao na hivyo wananchi kuona yale ambayo serikali inayafanya kwa maana ya kuleta maendeleo katika nchi.
Ameongeza kuwa, katika mkoa wa Arusha wana miradi mikubwa mitatu ya kitaifa mojawapo ni mradi wa kutoka Arusha Moshi mpaka Holili ambao utafadhiliwa na serikali ya Japan na mwingine ni mradi wa kiwanja cha ndege cha Manyara na nyingine ni ujenzi wa barabara kutoka Arusha kwenda Kibaya ambapo katika mradi huo kilometa 70 zipo ndani ya mkoa wa Arusha.
“Moja ya miradi ambayo inaendelea mkoa wa Arusha ni ujenzi wa uwanja wa ndege wa Lake Manyara ambao upo katika wilaya ya Karatu mradi huo unafadhiliwa chini ya mpango wa ujenzi unaofadhiliwa na Benki ya dunia ambazo ni miradi iliyowekwa kusaidia ukuzaji wa miundombinu ya barabara na viwanja vya ndege ,hivyo mkoa wa Arusha umenufaika kwa uwanja huo wa Lake Manyara .”amesema Mhandisi Besta.
“Utaona kuwa miradi inaendelea mbali na miradi mingine ambayo kutokana na mvua zisizo za kawaida za elinino za mwaka 2023/2024 na baadaye hata 2024/2025 serikali kupitia benki ya dunia ilipata fedha ambazo ni takribani shs bilioni 14 ambazo zimeenda kufadhili ujenzi wa makalavati na madaraja mawili kwani katika mkoa wa Arusha tumenufaika na hiyo katika barabara ya Arusha Namanga na katika barabara kuu kutoka Arusha kwenda kia ambapo ndo kuna mpaka katika mkoa wa Arusha .”amesema.
Ameongeza kuwa,serikali ipo macho na itaendelea kufanya kazi kwa bidii na wananchi ili kuhakikisha kuwa wanaona zile kazi ambazo taasisi ya TANROADS inaendelea kuzifanya.
“Tunahitaji kuendelea kuimarisha barabara zetu za mkoa wa Arusha na serikali kupitia mfuko wa barabara na kupitia katika miradi mbalimbali inayoendelea tuhakikisha kwamba mkoa wa Arusha ni mkoa wa kivutio kwa maana ya utalii na tuhakikishe kwamba miundombinu zetu ya barabara inaendela kuwa imara na hivyo kuendelea kuvutia watalii na kukuza uchumi wa Taifa na uchumi wa Arusha kwa ujumla .”amesema.
Kwa upande wake Meneja wa TANROADS mkoa wa Arusha , Mhandisi Reginald Massawe amesema kuwa Arusha ni mkoa wa kimkakati na ni mkoa uliopo katika kanda ya utalii na sisi kama TANROADS tunahudumia mtandao wenye kilometa 1,490 kati ya kilometa hizi asilimia 70 ya mtandao unapita katika mbuga zetu za wanyama.
“Mkoa umejipanga vizuri tuna miradi ya kimkakati ambayo sasa inaendelea ambapo mradi mkubwa uliopo sasa hivi ni mradi wa kuanzia Arusha -Moshi -Holili ambao unajengwa kwa njia nne na sasa hivi wapo katika awamu ya kujenga kutoka Tengeru mpaka Usa river lengo kubwa la kupanua barabara hiyo kwa njia nne ni msongamano mkubwa wa magari hasa malori ya mizigo yanayotoka katika bandari ya Tanga na bandari ya Mombasa kwenda nchi jirani za Ruanda .”amesema Meneja.
“Hivyo serikali imeona ni vizuri tupanue barabara hii ili watalii wanapotoka uwanja wa ndege wa KIA kuja Arusha wafike haraka na barabara iwe salama kwani barabara inapokuwa nyembamba ajali zinakuwa nyingi .”amesema Massawe.
Mhandisi Massawe amesema kuwa wanaenda kujenga barabara kutoka Mto wa mbu kwenda Loliondo ambapo barabara hii inapita katika mbuga ya Serengeti na kwenda kwenye vivutio vya Natron tayari na wameshaanza kilometa 49 kutoka Waso kwenda Sale zimekamilika na tunamshukuru Mtendaji mkuu wa TANROADS tumeshaini mkataba wa kilometa 10 kutoka Waso kwenda Loliondo na Tenda kutoka Mto wa mbu mpaka Engaruka zilishatangazwa na tupo katika hatua za mwisho za manunuzi na barabara hiyo ikifunguka itafungua utalii mkubwa sana kutoka Mto wa mbu kwenda Serengeti.
Ameongeza kuwa, wanaenda kufungua pia ukanda wa kusini kwenda Dodoma kwa barabara kubwa ya kutoka Arusha Kibaya kongwe kuna kilometa 70 ambazo zitaanza kujengwa Mbauda mpaka Losiilai mpakani mwa mkoa wa Manyara na barabara hiyo itakuja na mzunguko tena kurudi Moshono kwa hiyo itafungua pia ukanda wote wa Losilai hizo ni fursa kwani watu watajenga viwanja watapata na hivyo tumeona ni fursa tuje kusema katika Tamasha la Samia Connection kuonekana serikali inafungua maeneo mengi ya mkoa wetu ili wananchi waweze kwenda kule na kuweza kufanya shughuli zao ikiwemo biashara,viwanda na fursa zingine.
Ameongeza kuwa ,kwa upande wa utalii tunaenda kujenga uwanja wa ndege wa Lake Manyara kwani wakati wa mvua ulikuwa haufanyi kwani ulikuwa wa Changarawe hivyo wakati wa mvua ndege zilikuwa haziwezi kutua lakini kama.mnaoona utalii kwa mwaka huu umeongezeka kwa kiwango kikubwa katika mkoa wa Arusha hivyo tunaujenga uwanja ule kwa kiwango cha Lami ili wakati wa mvua ndege ziendelee kutua na watalii wataweza kwenda katika mbuga zetu kwa muda uliopangwa.
Kwa upande wa mwananchi aliyetembelea banda hilo amesema kuwa ,amewasifu TANROADS kwani wanajitahidi sana katika utekelezaji wa miradi mbalimbali kwa mfano barabara ya Minjingu mwanzoni ilikuwa barabara ambayo haipendezi ulikuwa unatembea kwa muda mrefu kwenda Singida na Kondoa ila kwa sasa hivi imerahisisha sana swala la usafiri kwani unafika kwa muda mfupi na muafaka.
Aidha ameomba TANROADS kuwaongezea kipande kidogo kwa kule sehemu ambazo zina mavumbi zifanyiwe kazi ili ziwe kiwango cha lami.