Na Mwamvua Mwinyi, Kibaha
Aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kibaha Vijijini (2020-2025), Michael Mwakamo, amewataka watu kuacha upotoshaji na upambe kuhusu madai kuwa ana mpango wa kuhama Chama cha Mapinduzi (CCM), akisisitiza kuwa ataendelea kuwa mwanachama mwaminifu wa chama hicho, na kwamba kwake, kurudi nyuma ni mwiko.
Akizungumza na vyombo vya habari Agosti 28, 2025, Mwakamo alieleza hana kinyongo na matokeo ya mchakato wa uteuzi wa ubunge, na kwamba haitakuwa na maana yoyote kwake kukisaliti chama kwa sababu tu hakupata nafasi ya kugombea tena.
“Nimetumikia umma kwa miaka 21, ikiwemo miaka mitano nikiwa Mbunge wa Kibaha Vijijini, Itakuwa ajabu kuondoka kwa sababu tu ya kukosa uteuzi, Navishukuru vikao vya maamuzi kwa kufanya kazi yao.
“Nampongeza Mbunge aliyepitishwa kupeperusha bendera ya CCM, nimepokea matokeo kwa furaha”; Sina hasira, na ukimya wangu usiwatie watu wasiwasi” alisisitiza Mwakamo.
Aliongeza kuwa ataendelea kushiriki kikamilifu katika kampeni zote za CCM na kuahidi kulitumikia chama kwa moyo wote.
“Siwezi kuondoka CCM kwa sababu ya kukosa nafasi ya kugombea ubunge, Chama chetu kina taratibu zake,Vikao vya maamuzi vya wilaya, mkoa na Taifa vimemaliza kazi yake, Sasa ni wakati wa kushikamana na kuhakikisha ushindi wa kishindo kwa CCM katika ngazi zote Urais, Ubunge na Udiwani,” alisisitiza.
Mwakamo pia alielezea mafanikio yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mgombea Urais kwa tiketi ya CCM, Dkt. Samia Suluhu Hassan, akisema:
“Dkt. Samia amefanya mambo makubwa ndani ya miaka minne — kuboresha sekta ya elimu, afya, barabara, umeme na mazingira ya wanafunzi wa kike. Hatuna la kumdai; bali yeye anatudai sisi tuendelee kumuunga mkono.”
Aidha, Mwakamo aliwaasa baadhi ya watu anaowaita “wapambe” na “machawa” kuacha uzushi, fitna na upotoshaji unaolenga kuwagombanisha waliogombea nafasi mbalimbali ndani ya chama.