*Vibali vya ujenzi wa vituo vya CNG kutolewa haraka ili kuvutia wawekezaji
*Taasisi za kifedha zashauriwa kutoa mikopo kwa wawekezaji kwenye sekta ya gesi
*Kituo cha Puma Tegeta kuwa kituo kikubwa zaidi cha CNG Jijini Dar es Salaam na Afrika
*Serikali kuanza kutumia magari yanayotumia gesi ya CNG badala ya dizeli na petroli.
Dar es Salaam, Agosti 29, 2025
Katika juhudi za kuiwezesha Tanzania kupiga hatua katika matumizi ya gesi asilia iliyoshindiliwa (CNG) kwa ajili ya magari, Serikali kupitia Wizara ya Nishati inaendelea kuimarisha upatikanaji wa miundombinu muhimu, ikiwemo ujenzi wa vituo vipya vya kujaza gesi kwenye magari katika maeneo mbalimbali.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dkt. James Mataragio, ameeleza hayo wakati wa ziara ya ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa vituo vya CNG Jijini Dar es Salaam.
“Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na taasisi ya Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC), Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na maji safi (EWURA) na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) imeweka mikakati madhubuti kuhakikisha usambazaji wa gesi ya CNG unafanyika kwa kasi, ikiwemo kuboresha mfumo wa utoaji wa vibali vipya vya ujenzi wa vituo ili vipatikane haraka,” alisema Dkt. Mataragio.
Alisisitiza kuwa hatua hiyo inalenga kuwavutia wawekezaji wengi zaidi na kuharakisha upatikanaji wa huduma hiyo katika maeneo mbalimbali nchini.
Aidha, alibainisha kuwa dhana iliyokuwepo awali miongoni mwa baadhi ya wawekezaji kuwa uwekezaji kwenye sekta ya nishati ni wa gharama kubwa na wenye hatari imeanza kubadilika, kufuatia juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali kuhamasisha uwekezaji wa ndani na nje.
Vilevile, alizihimiza taasisi za kifedha, hususan benki, kuendelea kutoa mikopo kwa wawekezaji waliopo katika sekta ya gesi, akisisitiza kuwa soko lina mahitaji makubwa na urejeshaji wa mikopo hiyo utakuwa rahisi kutokana na faida inayopatikana katika biashara hiyo.
Katika ziara hiyo, Dkt. Mataragio alikagua maendeleo ya ujenzi wa vituo vya CNG vilivyopo maeneo ya Tegeta (Puma), Goba (BQ)na Tanzania State Natural Gas), Mwenge (Enego Energies), Tan Health (Africana) na kituo cha TPDC kilichopo Hospitali ya Taifa Muhimbili ambacho ujenzi wake umekamilika, pia amesema kuwa vituo hivyo vinajengwa na wakandarasi Wazawa
Alieleza kuwa ujenzi wa vituo hivyo uko katika hatua za mwisho, na vinatarajiwa kukamilika kabla ya mwisho wa mwaka huu. Kati ya vituo hivyo, kituo cha Tegeta kinachosimamiwa na Kampuni ya Puma kimetajwa kuwa kitakuwa kituo kikubwa zaidi Jijini Dar es Salaam na Afrika, chenye uwezo wa kuzalisha futi za ujazo milioni 6.7 za gesi ya CNG kwa siku.
Pamoja na hayo, Dkt. Mataragio alisisitiza dhamira ya Serikali kuhamasisha wananchi kuachana na magari yanayotumia dizeli na petroli, na badala yake kuanza kuagiza magari yanayotumia gesi asilia.
“Tunaamini matumizi ya gesi ni ya gharama nafuu na salama kwa mazingira, na yanaleta tija kwenye taifa. Wizara ya Nishati itakuwa mfano kwa taasisi nyingine za serikali kwa kutumia magari yanayoendeshwa kwa gesi ya CNG,” aliongeza.
Aidha Dkt. Mataragio amesema wizara ya itaandaa warsha ya kuwakutanisha wadau wote wanaohusika katika Biashara ya CNG ikiwemo taasisi za kifedha, Wawekezaji ( Sekta binafsi) na taasisi za umma ili kuwajengea uweelewa kuhusu Biashara ya CNG na Min LNG.
Ziara hiyo ilihudhuriwa pia na wataalamu kutoka Wizara ya Nishati na Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC)