
Na Baltazar Mashaka, Misungwi
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru 2025, Ismail Ali Ussi, amevutiwa na kupongeza uwekezaji wa hosteli ya kisasa kwa ajili ya wanafunzi, uliofanywa na mwekezaji wa ndani Herman Batiho, kwa gharama ya shilingi milioni 894, wilayani Misungwi.
Ussi alitoa pongezi hizo leo, wakati wa uzinduzi wa mradi huo katika eneo la Nyang’homango, ambapo hosteli hiyo inayojulikana kwa jina la Double M imejengwa kwa ajili ya kuhudumia wanafunzi wa Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA),Kampasi ya Mwanza.
“Umeweka matumaini makubwa kwa serikali. Wilaya itakuunga mkono kwa uwekezaji huu wa kizalendo na wa kuwajali watoto wa wananchi wenzako. Umeiheshimisha Halmashauri ya Wilaya ya Misungwi kwa maendeleo , ungeweza kusema ubaki na fedha zako, lakini umeamua kuwajali wengine,” alisema Ussi .
Aliongeza kuwa mradi huo ni mfano hai wa utekelezaji wa maono ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye aliahidi kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji wa ndani na nje, huku akisisitiza kuwa serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi katika kukuza elimu na huduma nyingine muhimu kwa wananchi.
“Kupitia wanahabari hawa, Rais Dkt. Samia ataona jinsi ambavyo maono yake yanavyotafsiriwa kwa vitendo. Vijana watakaopanga na kuishi katika hosteli hizi watalipa kodi, halmashauri itanufaika kwa mapato, na Misungwi itajengwa na wana Misungwi wenyewe,” alisema Ussi.
Akizungumzia mradi huo, Herman Batiho alisema aliamua kuwekeza baada ya kubaini changamoto ya wanafunzi kukosa huduma ya malazi, kufuatia serikali kujenga chuo cha TIA katika eneo hilo.
“Tuliona fursa kubwa kwa vijana wanaokuja kusoma, lakini hawakuwa na sehemu ya kupanga. Uongozi wa chuo ulihamasisha watu wenye uwezo kuwekeza kwenye hosteli. Tuliitikia wito huo Aprili mwaka jana ili kuunga mkono juhudi za serikali katika utoaji wa elimu ya juu,” alieleza.
Batiho aliongeza kuwa hosteli ya Double M ina uwezo wa kuhudumia wanafunzi 200 kwa wakati mmoja, na imejengwa kwa ubora wa hali ya juu ili kutoa mazingira salama na rafiki kwa masomo.
Aliwataka wanafunzi watakaoishi katika hosteli hiyo kutunza miundombinu kwa ajili ya vizazi vijavyo, huku akibainisha kuwa mradi huo pia utasaidia kuongeza mapato ya serikali kupitia kodi mbalimbali.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Misungwi, Johari Samizi, alimshukuru Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuridhia ujenzi wa chuo hicho cha TIA wilayani humo.
Alisema uwekezaji wa hosteli hiyo umetokana moja kwa moja na ujio wa taasisi hiyo ya elimu ya juu, na ni ishara kuwa Misungwi inazidi kufunguka kiuchumi na kielimu.
Uwekezaji wa Batiho kupitia hosteli ya Double M sio tu unachangia maendeleo ya sekta ya elimu wilayani Misungwi, bali pia unaunga mkono ajenda ya taifa ya kutoa elimu bora na kuongeza fursa kwa vijana.