Na Angela Msimbira , OR–TAMISEMI
Naibu Katibu Mkuu anayeshughulikia TAMISEMI, Ofisi ya Rais – Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR–TAMISEMI), Sospeter Mtwale, amewataka maafisa bajeti wa Sekretarieti za Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa kuhakikisha bajeti zinazotayarishwa zinakaguliwa na kuthibitishwa usahihi wake kabla ya kuwasilishwa kwenye ngazi za juu za maamuzi.
Akifungua mafunzo ya uandaaji na utekelezaji wa mipango ya bajeti leo, Septemba 2, 2025, mjini Dodoma, Mtwale amesema ni wajibu wa maafisa bajeti kufuatilia taarifa za utekelezaji wa bajeti kila robo mwaka na kuwasilisha kwa wakati kwa kuzingatia mwongozo wa serikali.
“Ni lazima maombi yote ya upungufu wa bajeti katika mamlaka za Serikali za Mitaa yahakikiwe usahihi wake kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti, Sura ya 436, kabla ya kuwasilishwa katika Ofisi ya Rais – TAMISEMI,” amesema Mtwale.
Aidha, amewataka maafisa bajeti hao kuhakikisha mipango ya bajeti inaandaliwa kwa kuzingatia miongozo ya serikali, kufanyika ufuatiliaji wa utekelezaji wake kwa kushirikiana na idara mbalimbali, na kutoa mafunzo kwa maafisa waliopo katika ngazi zao ili kuongeza ufanisi.
Awali, akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi wa Mamlaka za Serikali za Mitaa, Ofisi ya Rais – TAMISEMI, Kassim Mudrika Kassim Mjungu, alisema mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo maafisa bajeti kutoka mikoa na halmashauri mbalimbali wakiwemo wachumi, maafisa mipango na watakwimu.
Amefafanua kuwa mafunzo hayo yatasaidia kuongeza umahiri katika hatua muhimu za uandaaji wa bajeti, matumizi ya mifumo ya kitaifa kama PlanRep, na kuboresha mipango ya bajeti kulingana na mahitaji ya serikali na jamii.