
Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) umeionya Israel kwamba mpango wa kutwaa kwa mabavu maeneo ya Ukingo wa Magharibi utavunja mipaka na kudhoofisha ari ya Mkataba wa Abraham, uliorejesha uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili mwaka 2020.
Afisa Mkuu wa Imarati katika Umoja wa Mataifa, Lana Nusseibeh, amesema hatua hiyo “itakuwa mwisho wa matumaini ya suluhisho la mataifa mawili” katika mzozo wa muda mrefu kati ya Israel na Palestina.
Kwa upande wake, Wizara ya Mambo ya Nje ya Mamlaka ya Ndani ya Palestina imetangaza kuunga mkono msimamo wa UAE, ikisema unathibitisha uhalali wa madai ya Wapalestina dhidi ya upanuzi wa Israel.
Israel haijatoa kauli rasmi. Hata hivyo, onyo la Imarati limeibuka siku chache baada ya Waziri wa Fedha wa Israel mwenye msimamo mkali, Bezalel Smotrich, kufichua pendekezo la kutwaliwa kwa takriban theluthi tatu ya eneo la Ukingo wa Magharibi.
Tangu Israel kuikalia kwa mabavu ardhi hiyo pamoja na Jerusalem Mashariki katika vita vya Mashariki ya Kati vya mwaka 1967, imejenga zaidi ya makazi 160 yenye idadi ya takriban Wayahudi 700,000. Eneo hilo pia ni makazi ya karibu Wapalestina milioni 3.3, ambao wanalitazama, pamoja na Gaza, kama msingi wa taifa huru la Palestina.