Na Mwamvua Mwinyi, Pwani
Jeshi la Polisi mkoani Pwani linamshikilia kijana mmoja aitwaye Ally Juma Shaban (29), mganga wa tiba asilia na mkazi wa Makazi Mapya, Mlandizi, kwa tuhuma za mauaji ya Juma Yoram Nyambihira (58), mkazi wa eneo hilo hilo.
ACP Muhudhwari Msuya, Kaimu Kamanda wa polisi mkoani Pwani, alithibitisha kuwepo kwa tukio hilo.
Alisema, agost 29 ,2025, Jeshi la Polisi katika Kituo cha Polisi cha Mlandizi lilipokea taarifa kutoka kwa ndugu wa marehemu wakieleza kuwa ndugu yao, Juma Nyambihira, alikuwa hajulikani alipo tangu 17 Agosti 2025.
Baada ya kupokea taarifa hizo, polisi walifungua jalada la uchunguzi na kuanza ufuatiliaji wa kina.
Katika uchunguzi huo, Ally Juma Shaban alikamatwa, ambaye inadaiwa alikuwa akiishi na marehemu na ndiye aliyekuwa akimhudumia kwa matibabu ya tiba asilia kutokana na matatizo ya uoni hafifu yaliyokuwa yakimkabili marehemu.
Mnamo Septemba 3, 2025, wakati upelelezi ukiendelea, askari wa Jeshi la Polisi walifika nyumbani kwa mtuhumiwa kwa ajili ya upekuzi wa kina, katika maeneo ya karibu na nyumba hiyo, walikuta tanuri la kuchomea mkaa, ambapo kulionekana dalili za moshi.
Baada ya kufanya uchimbaji katika eneo hilo, walifanikiwa kuupata mwili wa marehemu ukiwa umezikwa ndani ya tanuri hilo. Mwili huo umekabidhiwa kwa daktari kwa ajili ya uchunguzi wa kitabibu kabla ya kukabidhiwa kwa familia kwa taratibu za mazishi.
Jeshi hilo linakemea vikali tukio hilo na limewahakikishia wananchi kuwa linaendelea kuimarisha usalama wa raia na mali zao.