*Aacha matumaini makubwa kwa wakulima wa zao la parachichi ,Chai wilayani Rungwe
*Mashamba ambayo wawekezaji wameshindwa kuyaendeleza Serikali yaunda timu kufuatilia
Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Rungwe
KAMPENI za mgombea Urais kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suhusu Hassan zimeendelea katika Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya ambapo maelfu ya wananchi wamejitokeza kwenye mkutano huo.
Akiwa katika mkutano wa kampeni kuelekea Uchaguzi Mkuu Oktoba 29 mwaka huu Rais Dk.Samia Suluhu Hassan pamoja na mambo mengine amewahakikishia wakulima wa Rungwe na kote nchini kuwa Serikali katika miaka mitano ijayo itaendelea kuweka mazingira katika sekta ya kilimo.
Kwa upande wa Wilaya ya Rungwe mkoani Mbeya ,Dk.Samia ametumia nafasi hiyo kuzungumzia mashamba ambayo Serikali iliyatoa kwa wawekezaji kufanya uwekezaji katika kilimo na viwanda lakini baadhi ya mashamba wawekezaji wameshindwa kuyaendeleza.
“Kwa hapa Rungwe kuna wawekezaji ambao ni WETCO na Kampuni ya Mohammed Interprises ambao wamelalamikiwa kutolipa madeni ya wakulima na wafanyakazi wa viwanda vyao pamoja na kushindwa kuyaendeleza mashamba waliyopewa.
“Nikianza na hoja ya chai, najua kwenye chai kuna mtu anaitwa WATCO na Mohammed Interprises, ndugu zangu mashamba haya tuliyatoa tukiamini sekta binafsi tutafanyanayo kazi kwa ajili ya maendeleo ya watu.”
Ameongeza kuwa hivyo ndivyo inavyotokea maeneo mengi kwani Serikali imeamua kufanyakazi na sekta binafsi kwa lengo la kusaidiana katika kuleta maendeleo ya watu. Hivyo Serikali imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji kuanzia sheria, sera na mambo mengine.
Amefafanua kuwa walikubaliana na WETCO na Mohammed interprises kuwapa mashamba waweke viwanda ili chai iongezwe thamani kabla ya kusafirishwa, lakini inavyoonekana kazi hiyo imewashinda.
Hata hivyo katika hoja hiyo ya mashamba hayo kutoendelezwa amesema tayari Serikali imeunda timu ambayo inafanya tathmini ya mashamba na viwanda, lengo likiwa ni kuyachukua pamoja na viwanda kisha kumilikisha kwa vyama vya ushirika chini ya serikali.”
Dk.Samia amesema pia amesema anajua kwamba WETCO na Mohamed Interprises wanamadeni ya wafanyakazi wao wa viwanda lakini pia kwa wakulima. “Nataka niwaambie tumewaelekeza waanze kulipa madeni ya watu.”
Aidha mgombea huyo wa Urais ,Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema kuwa serikali imeweka mazingira mazuri kwa wawekezaji hao kupata mikopo katika taasisi za kifedha ili kulipa madeni hayo.
Hivyo amesisitiza madeni ya wakulima pamoja wafanyakazi wa viwanda lazima yalipwe kabla ya serikali haijachukua mashamba na kuwamilikisha wanaushirika.Majibu ya Rais Samia yameonekana kuwafurahisha wananchi wa Rungwe ambao kwa sehemu kubwa wanategemea kilimo cha parachichi pamoja na chai katika kukuza uchumi wao.
Pamoja na hayo amewapongeza wakulima wa zao la parachichi kwa kuongeza uzalishaji na kuifanya Tanzania kushika nafasi ya tatu duniani na kuongeza parachichi ya Tanzania imepata soko katika mataifa mbalimbali.
“Kama mnavyojua biashara bei inapanda na kushuka, kwenye chai hivyo hivyo soko la dunia limepanda halafu likashuka na ndiyo maana wawekezaji wakashindwa kuendeleza lakini serikali kama soko ni zuri au kama soko ni baya wajibu wetu ni kuwashika wakulima wetu na hicho ndicho tunachokwenda kufanya.
Amesema kuwa duniani wanazalisha parachichi lakini kwa bahati mbaya zinazalishwa wakati mmoja na ndiyo maana bei inashuka kwani wanunuaji wanakuwa na uwanja mpana wa kuchagua.
Hata hivyo amesema serikali katika miaka mitano ijayo ina mpango wa kujenga vituo 50 vya kuhifadhi zao hilo na viwanda vidogo vya kuongeza thamani ya parachichi.
Amesema katika vituo hivyo vya kuhifadhi parachichi vitakavyojengwa vituo viwili vitajengwa katika Wilaya Rungwe ambavyo vitakuwa na baridi ya kuhifadhia parachichi na mazao mengine ya mbogamboga.
Amesema lengo la kuwezesha kuhifadhi parachichi katika vituo hivyo ni kutoa nafasi wakati mataifa mengine yamezalisha parachichi na kuuza katika masoko basi parachichi za Rungwe na maeneo mengine ziwe zinavuta muda wakati zinasubiria soko.
“Wakulima na wanaushirika watauza katika vituo ambavyo vitakusanya, kuhifadhi kusubiri soko lipande bei.
Aidha amesema Serikali ina lengo la kujenga kongani ya viwanda katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo wilayani Rungwe.
Katika mkutano huo Rais Dk.Samia amesisitiza kwamba katika miaka
Mitano ijayo Serikali itakwenda kuongeza kasi ya kuleta maendeleo ya wananchi huku akiwaomba wananchi kuichgaua CCM katika Uchaguzi Mkuu unaokwenda kufanyika Oktoba 29 mwaka huu.