Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) leo imepokea wanafunzi wa kidato cha nne kutoka Shule ya Sekondari Baobab, kwa lengo la kuwapatia elimu kuhusu Taaluma ya Uhasibu na kazi mbalimbali zinazofanywa na Bodi hiyo.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius A. Maneno, Mkurugenzi wa Huduma za Shirika, CPA Kulwa Malendeja, alisema uhusiano kati ya NBAA na Baobab umekuwa wa muda mrefu na umesaidia kuongeza uelewa wa wanafunzi kuhusu kazi na nafasi ya Bodi katika kusimamia Taaluma ya Uhasibu nchini.
Amesisitiza kuwa kwa sasa Bodi hiyo inatumia mifumo ya kidijitali katika kutoa huduma zake kupitia tovuti yake rasmi, hatua inayolenga kurahisisha upatikanaji wa taarifa na kuongeza ufanisi.
Aliongeza kuwa hata wanafunzi wa kozi nyingine zisizohusiana moja kwa moja na uhasibu wana nafasi ya kuanza safari hiyo kwa kufanya mitihani ya ngazi ya kwanza (foundation level), huku waliomaliza kidato cha nne na sita wenye vyeti nao wakipewa nafasi ya kujisajili na kushiriki mitihani ya NBAA.
Naye Mkuu wa kitengo cha Rasilimali Watu NBAA, Gloria Kaaya amewaasa wanafunzi wa Baobab kusoma kwa bidii ili kufikia malengo yao kwani Taifa lina uhitaji sana wa wahasibu.
Amesisitiza kuwa na maadili ya msingi ili kufanya vyema katika masomo yao
Aidha, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa NBAA, Magreth Kageya aliongeza kuwa si kila aliyesomea uhasibu anakuwa mhasibu kitaaluma, bali ni wale pekee wanaofanya mitihani ya Bodi na kufaulu ndio hutambulika kama wahasibu au mkaguzi kwa kupatiwa cheti rasmi cha CPA kinachotambulika ndani na nje ya nchi.
Kwa upande wake, mwalimu wa Shule ya Sekondari Baobab, Stephen Gervas Mahundi, aliishukuru NBAA kwa kutoa elimu hiyo muhimu, akieleza kuwa itawasaidia wanafunzi kupata dira na mwelekeo bora katika maisha yao ya kitaaluma.
Picha ya pamoja ya baadhi ya menejimenti ya NBAA, watoa mada, walimu pamoja na wanafunzi wa Baobab

Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa NBAA, Magreth Kageya akitoa ufafanuzi kuhusu kazi zinazofanywa na bodi hiyo wakati wa mafunzo kwa wanafunzi wa Kidato cha nne kutoka Shule ya Sekondari ya Baobab.
Mkaguzi wa ndani wa NBAA, CPA George Lazaro akitoa elimu kuhusu kazi za Wahasibu na Wakaguzi kwa wanafunzi wa Kidato cha nne kutoka Shule ya Sekondari ya Baobab waliotembelea na kupata mafunzo katika ofisi za Bodi ya NBAA.
Mkuu wa kitengo cha Rasilimali Watu NBAA, Gloria Kaaya akizungumza wakati wa kufunga mafunzo ya wanafunzi wa Kidato cha nne kutoka Shule ya Sekondari ya Baobab.
Mwalimu wa Shule ya Sekondari ya Baobab Stephen Gervas Mahundi akitoa neno la shukrani kwa uongozi wa Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi Hesabu Tanzania (NBAA) mara baada ya kumaliza ziara yao walipotembelea ofisi za Bodi ya NBAA
Baadhi ya wanafunzi wa Kidato cha nne kutoka Shule ya Sekondari ya Baobab wakifuatilia mada mbalimbali zilizowasilishwa na wataalam kutoka Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu (NBAA) walipotembelea ofisi za Bodi hiyo zilizopo jijini Dar es Salaam.