Kamishna Idara ya Michezo Zanzibar Ameir Mohammed Makame akizungumza na Wadau wa Mpira wa Wavu wakati wa hafla ya kujitambulisha katika Ukumbi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Migombani Wilaya ya Mjini.
…………….
Kamishna Idara ya Michezo Zanzibar, Ameir Mohammed Makame amesema Ushirikiano wa Wadau wa Mpira wa Wavu, utasaidia kuimarisha mashindano ya kikanda, kitaifa na kimataifa.
Aliyasema hayo, wakati wa hafla fupi ya kujitambulisha na kukuza mashirikiana ya Taasisi mbalimbali za Mpira wa Wavu huko katika Ukumbi wa Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Migombani Wilaya ya Mjini.
Ameeleza kuwa, kuimarika kwa mashirikiano hayo kutasaidia kukuza vipaji vya michezo Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Aidha, aliongeza kuwa, kufanyika kwa mashindano ya Michezo hapa Nchini pia itasaidia kuendeleza Vijana na kuitangaza Zanzibar kiutalii katika anga za kitaifa na kimataifa.
Nae Kiongozi wa Ujumbe huo, Bw. Oliver kutoka Ujerumani amesema lengo la ziara hiyo ni kuangalia miundombinu ya Viwanja na kutoa mafunzo kwa wanamichezo ili viweze kutumika kwa mashindano makubwa.
Aidha amesema ziara hiyo, itasaidia kuibuwa vipaji mbalimbali vya Vijana na kuweza kushiriki katika mashindano ya kimataifa yanayotarajiwa kufanyika Zanzibar mwaka 2028.
Kwa Upande wa Mchezaji wa Mpira wa Wavu ambae alishiriki katika Mashindano ya Rwanda na Burundi Abass Makame Ussi kutoka Zanzibar ameiomba Serikali kuendelea kuimarisha Mashindano ya Mchezo huo ili kupata vigezo vya kushiriki mashindano ya kimataifa.
Ujumbe huo, wenye lengo la kuangalia Miundombinu ya Mpira huo na kutoa Mafunzo kwa Viongozi na Wachezaji wa Mpira wa Wavu, umehusisha Vilabu mbalimbali kutoka Ujerumani, Mwakilishi wa Faru Sports Foundation ya Dar-es-salaam pamoja na Shirikisho la Mpira wa Wavu Zanzibar.