
Mahakama mjini Johannesburg imewahukumu raia saba wa China kifungo cha miaka 20 jela kila mmoja kwa makosa ya usafirishaji haramu wa binadamu na kuwalazimisha raia 91 wa Malawi kufanya kazi katika kiwanda cha nguo bila masharti ya kibinadamu.
Wachina hao walikamatwa mwaka 2019 baada ya polisi kuvamia kiwanda chao kilichozungukwa ukuta mkubwa na waya wa miiba, na kuwakuta wafanyakazi wakilindwa na walinzi wenye silaha.
Waathiriwa walieleza walivyolazimishwa kufanya kazi saa 11 kila siku, bila chakula sahihi, bila vifaa vya usalama, na bila ruhusa ya kuwasiliana na watu wa nje. Mashahidi walidai pia walifanyishwa kazi hata siku za mapumziko huku wakiwa wamefungwa ndani ya kiwanda.
Waendesha mashtaka walitaka wahukumiwe kifungo cha maisha, wakisisitiza unyama wa mateso waliyopitia wahanga.