NA JOHN BUKUKU- KASULU KIGOMA
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameahidi kukamilisha mradi mkubwa wa kufua umeme wa maji katika Mto Malagarasi, mradi unaotarajiwa kuzalisha megawati 49.5 na kuokoa zaidi ya shilingi bilioni 58 ambazo zingetumika kusafirisha umeme kutoka mbali.
Akizungumza kwenye mkutano wa kampeni mkoani uliofanyika wilayani Kasulu mkoani Kigoma, Dkt. Samia alisema bwawa hilo ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kitaifa yenye lengo la kuhakikisha Kigoma inapata umeme wa uhakika, jambo litakalosaidia kusukuma gurudumu la maendeleo na kufungua fursa nyingi za uwekezaji.
“Mradi wa bwawa la Malagarasi utarahisisha usambazaji wa umeme ndani ya vijiji vyetu. Tutajenga pia kituo cha kupooza umeme na kuhakikisha kila kitongoji kinapata huduma hii muhimu. Hii itasaidia vijana, wakulima na wajasiriamali kufanya kazi kwa ufanisi zaidi,” alisema Dkt. Samia.
Aidha, alibainisha kuwa uwepo wa umeme wa uhakika utasaidia kuimarisha viwanda vilivyopo Kigoma, ikiwemo viwanda vya saruji na sukari, pamoja na kuvutia wawekezaji wapya kuanzisha viwanda vingine vitakavyoongeza ajira na pato la wananchi.
Sambamba na mradi wa umeme, Dkt. Samia aliahidi kuboresha mtandao wa barabara za Kasulu zilizomo kwenye Ilani ya CCM 2025–2030, ikiwemo barabara ya Mwanga–Kasulu–Muyamba yenye urefu wa kilomita 36 na barabara ya Uvinza–Kanyani yenye urefu wa kilomita 60 na nyingine ambazo zitajengwa kwa kiwango cha lami. Aliongeza kuwa barabara zingine muhimu zitaanza kwa kiwango cha changarawe ili wananchi wasipate kikwazo cha usafiri wakati wote wa mwaka.
Barabara zinazojulikana zikihusiana na Kasulu na mkoa wa Kigoma kwa ujumla. Kuna barabara ya Uvinza – Malagarasi yenye kilomita 51.1 ambayo ipo kwenye ujenzi wa kiwango cha lami. Pia ipo barabara ya Kabingo – Kasulu – Manyovu yenye kilomita 260.6, na sehemu ya Kasulu – Manyovu yenye kilomita 68.25. Upande mwingine kuna barabara ya Kanyani – Kidyama – Mvugwe yenye kilomita 70.5 pamoja na barabara ya Mvugwe – Nduta Junction yenye kilomita 59.35. Aidha, barabara ya Nduta Junction – Kabingo yenye kilomita 62.50 pia ni sehemu ya mtandao wa barabara zinazoboreshwa. Sambamba na hizo, barabara ya Buhigwe – Kasulu – Manyovu ambayo ni sehemu ya kipande cha Kabingo – Kasulu – Manyovu (takribani kilomita 56) imekusudiwa pia kujengwa kwa kiwango cha lami.