Na John Bukuku, Dar es Salaam
Huduma ya usafiri kwa treni ya kiwango cha kimataifa ya Standard Gauge Railway (SGR) imechukua sura mpya baada ya sekta binafsi kutarajiwa kuanza kutoa huduma ya kusafirisha abiria kwa mabasi kutoka Stesheni za Morogoro na Dodoma kuanzia Septemba 15, 2025.
Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Septemba 13, 2025, Kaimu Mkurugenzi wa Kurugenzi ya Maendeleo ya Biashara wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Bw. Frederick Massawe, alisema ushirikiano huo ni sehemu ya mkakati wa TRC kuhakikisha huduma za usafiri wa reli zinakuwa jumuishi, bora na zinazohusisha sekta binafsi ili kukuza huduma na fursa za kiuchumi.
Bw. Massawe alisema hatua hiyo pia ni utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya kuendeleza ubia kati ya sekta ya umma na binafsi kwa manufaa ya wananchi na maendeleo ya Taifa. Alibainisha kuwa, ushiriki wa sekta binafsi unafuatia mabadiliko ya Sheria Na. 10 ya mwaka 2017 iliyounda TRC, yaliyofanywa na Serikali mwaka 2023 na kusainiwa na Rais, hivyo kutoa fursa za kiundeshaji kwa watu binafsi.
Kwa upande wake, Msemaji Mkuu wa Kampuni ya Faima, Bi. Saphina Abraham, alitaja ruti za mabasi katika Mkoa wa Morogoro kuwa ni Viwandani, Stendi ya Msamvu, Masika na Stendi ya zamani ya mabasi. Aidha, kwa upande wa Dodoma vituo vitakuwa Kituo cha Mabasi Nanenane, Machinga Complex na Shoppers Plaza.
Bi. Saphina aliongeza kuwa, huduma hiyo kwa kuanzia imezalisha jumla ya ajira 61, ikiwemo wahudumu 32, madereva 26 na wasimamizi watatu. Alisisitiza kuwa ajira hizo ni mchango mkubwa katika kuchangia kipato cha mtu mmoja mmoja, familia na Taifa kwa ujumla.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Faima General Supply Company Limited, Bw. Ceaser Amani, alisema kampuni yake imejipanga kutoa huduma bora na za kiushindani ili kusaidia wananchi kufurahia zaidi manufaa ya uwekezaji mkubwa uliofanywa na Serikali kupitia reli ya kisasa ya SGR.