NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
Zaidi ya washiriki 15 kutoka sekta mbalimbali za afya wanatarajiwa kushiriki na kujadili mada muhimu zikiwemo lishe, tiba ya viungo, afya ya akili, afya ya uzazi, pamoja na afya ya kinywa na macho.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Septemba 15, 2025 Jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa shirika lisilo la kiserikali Masaki Wellspring Hub, Fortunatus Ekklesiah, amesema kuwa lengo la Masaki Wellspring Hub ni kuona watu wanaishi maisha yenye afya kamili,
Aidha amewataka wakazi wa Dar es Salaam kuhudhuria kwa wingi, akisisitiza umuhimu wa familia kushiriki kwa pamoja.
“Tumeandaa vitu kwa ajili ya kila mmoja, elimu ya afya si suala la mtu binafsi pekee bali ni msingi wa maendeleo ya kiuchumi, tumezingatia mada za afya zinazogusa moja kwa moja maisha ya kila siku na ustawi wa jamii.” Amesema
Kwa upande wake Mratibu wa Tiba wa Manispaa ya Kinondoni, Dkt. Omary Mwangaza amesema expo hiyo inalenga kuongeza uelewa kwa wananchi kupima na kutambua afya zao mapema kabla ya kushtukizwa na matokeo ya ugonjwa, sambamba na kuunga mkono programu ya afya ya msingi iliyozinduliwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Tamisemi.
“Kwa kuwa huduma hizi zitatolewa bila gharama, ni jambo la kupongezwa. Nawakaribisha wakazi wa Dar es Salaam na maeneo jirani kuhudhuria siku ya tarehe 21 ya mwezi huu,” Amesema
Amesema kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika mapambano dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza (NCDs) ambayo hivi sasa yanasababisha vifo kwa kiwango kikubwa zaidi kuliko magonjwa ya kuambukiza nchini.
Nae Mkurugenzi wa Shirika lisilo la kiserikali la Tanzania Oral Heath Foundation, Dkt. Winfred Mgaya amesema kupitia Expo hiyo watashiriki katika kutoa huduma ya elimu na uchunguzi wa afya ya kinywa na meno kwa jamii nzima ambayo wataweza kufika katika maonesho hayo.
Tukio hilo limeandaliwa kwa ushirikiano na London Health Centre, Genzero Sickle Cell 2050, Halmashauri ya Manispaa ya Kinondoni na wadau wengine wa afya, ambapo zaidi ya wakazi 200 wa Masaki wanatarajiwa kushiriki.
