15 Septemba 2025, ARUSHA
Waajiri nchini wametakiwa kuweka utaratibu wa kuwajengea uwezo watumishi wao kwa kuwapatia mafunzo mara kwa mara yatakayowawezesha kuwa na uelewa wa pamoja ili kuepusha migogoro sehemu za kazi.
Wito huo umetolewa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana na Wenye Ulemavu, Bi. Zuhura Yunus alipokuwa Mgeni Rasmi katika Ufunguzi wa Semina ya Waajiri na Viongozi wa Matawi ya TUGHE uliofanyika leo Jumatatu tarehe 15 Septemba 2025 Katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa AICC Jijini Arusha
“Watumishi pamoja na Waajiri wakielewa vyema Taratibu, Miongozo, Sheria na Kanuni zinazosimamia Utumishi wa Umma na masuala ya ajira na mahusiano kazini kwa ujumla wake, haitakuwa rahisi wao kuzikiuka. Mara nyingi Watumishi na Waajiri wanatenda makosa kwa kutotambua kuwa wanakosea” Alieleza Bi. Yunus
Katika hatua nyingine Bi. Zuhura Yunus amewaonya baadhi ya Waajiri Nchini kuacha tabia ya kuwazuia watumishi haki yao ya kujiunga na vyama vya wafanyakazi kwani ni ukiukwaji wa haki zao na kubainisha kuwa Serikali haitasita kumchukulia hatua mwajiri yoyote atakayebainika kufanya kosa hilo.
Awali akitoa salamu za ukaribisho, Katibu Mkuu wa TUGHE, Cde. Hery Mkunda ameeleza kuwa Idadi ya washiriki wa Semina imekuwa ikiongezeka kila mwaka ambapo kwa mwaka huu TUGHE inatarajia kutoa mafunzo kwa washiriki zaidi ya 800 kutoka katika Wizara, Idara, Taasisi, Wakala wa Serikali, Mamlaka za Serikali, Bunge, Mahakama, Sekretarieti za Mikoa, Mamlaka za Serikali za Mitaa na Taasisi za Afya za Serikali na zile za binafasi.
Cde. Mkunda amebainisha kuwa mafunzo haya yalianza kutolewa rasmi mwaka 2018 ambapo na yanakusudia kutoa elimu ya masuala mbalimbali ya kiutumishi kwa Waajiri na watumishi na wanachama wa TUGHE. Kuimarisha mahusiano mema baina ya Waajiri na Wafanyakazi sehemu za kazi ili kupunguza migogoro sehemu za kazi.
Ufunguzi wa Semina ya Waajiri na Viongozi wa Matawi ya TUGHE kwa mwaka huu 2025 yamehudhuriwa pia na Viongozi mbalimbali akiwemo Kamishna wa Kazi Mhe. Suzan Mkangwa, Jaji Mfawidhi Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Yose Mlyambina, Msajili wa Vyama vya Wafanyakazi na Waajiri, Mhe. Vallensi Wambali, Mkurugenzi Mkuu wa CMA, Mhe. Usekelege Mpulla, Mwenyekiti wa TUGHE Taifa, Cde. Joel Kaminyoge na Makamu Mwenyekiti TUGHE Taifa, Dkt. Jane Madete.
Mafunzo haya yatakayohitimishwa siku ya Alhamisi, tarehe 18/09/2025 kwa washiriki wote kufanya utalii wa ndani kwa kutembelea Mlima Kilimanjaro kasha wahitimu wote kupatiwa vyeti vya ushiriki.