Maneno hayo yamesemwa jana na Mgombea Mbunge jimbo la Chalinze Ndg. Ridhiwani Kikwete alipokuwa akinadi sera na ilani ya uchaguzi ya CCM mbele ya wanachalinze waliojitokea kwa wingi kwenye mkutano wa ufunguzi wa kampeni za uchaguzi wa Mbunge huyo katika mji wa Mdaula, Bwilingu.
Akiongea mbele ya wananchi hao Ndg. Kikwete ametumia nafasi ya jukwaa hilo kuwakumbusha wana chalinze ahadi za ilani ya CCM mwaka 2020 na jinsi ambavyo wamefanikiwa kutekeleza. Mgombea huyo amewakumbusha mambo sita ambayo yalikuwa ni kitendawili kwa wananchi hao ikiwemo shida kubwa ya maji, uchumi na makusanyo, afya, elimu na maendeleo ya jamii. Mgombea huyo wa Ubunge aliwaelexa wanachalinze mafanikio yaliyokwisha patikana huku akishukuru ushirikiano mkubwa na uongozi wa Rais Dr. Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha utekelezaji wa ilani hiyo kwa hali ya juu.
Kwa upande wa elimu , mgombea aliwakumbusha idadi ya shule mpya za msingi na sekondari, nyumba za walimu, ukarabati wa shule chakavu zilizojengwa na kufanyiwa ukarabati. Aliwakumbusha pia kwenye miradi ya afya hasa programu mbalimbali zilizofanyika jimboni ikiwemo pia ujenzi wa hospitali ya wilaya, Vituo vya Afya 6, zahanati 54 zilizokwisha jengwa, na kwa upande wa maendeleo ya jamii masoko, vituo vya afya, mikopo nk.
Mgombea kikwete alitumia jukwaa hili pia kuwakumbusha kuwa ilani ya CCM imeelekeza mambo mengi mazuri kufanyika ikiwa ni pamoja na kumalizia kazi ya kupeleka maji kwenye makazi ya wanachalinze, ujenzi wa mabweni na shule mpya , kilimo kitapewa kipaumbele, mifugo bora, chalinze ya viwanda, na mengineyo mengi.
Akizungumza kabla hajamkaribisha mgombea kuzungumza mgeni rasmi wa uzinduzi huo Bi. Zainab Vullu amewashukuru wanachalinze kwa ushirikiano mkubwa wanaompa mbunge wao na ndiyo maana mafanikio yanaonekana. Ametumia pia nafasi hiyo kuwaombea kura madiwani wa halmashauri hiyo na Mgombea urais wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano Dr. Samia Suluhu Hassan wa Chama Cha Mapinduzi.