
Familia na marafiki wa mwanariadha wa Kenya, Evans Kibet, wamesema wameshtushwa na taarifa kwamba mtoto wao amekamatwa nchini Ukraine akiwa upande wa vikosi vya Urusi.
Jeshi la Ukraine limetoa video ikimuonyesha Kibet, wakisema alikuwa anapigana kwa niaba ya Urusi. Katika rekodi hiyo, Kibet anadai alidanganywa kujiunga na jeshi la Urusi wakati alikuwa ameenda nchini humo kama mtalii.
Kwa mujibu wa simulizi yake, safari ya kwenda St. Petersburg iliandaliwa na wakala wa michezo na kufadhiliwa na serikali ya Urusi. Hata hivyo, anadai kuwa mwishoni mwa safari hiyo pasipoti na simu yake zilichukuliwa na kulazimishwa kusaini hati zilizoandikwa kwa lugha ya Kirusi bila kuelewa kilichoandikwa. Baada ya hapo, aligundua kwamba alikuwa ameandikishwa rasmi kama mwanajeshi.
Kibet anasema alipatiwa mafunzo ya kijeshi ya wiki moja na kukabidhiwa bunduki, lakini alikataa kushiriki vitani. Baada ya jaribio la kutoroka, alijificha msituni kwa siku mbili kabla ya kujisalimisha kwa wanajeshi wa Ukraine.
Katika video iliyotolewa na majeshi ya Ukraine, mwanariadha huyo anaomba asirudishwe Urusi akihofia maisha yake.
Hadi sasa, Serikali ya Urusi haijatoa tamko lolote kuhusu tukio hilo.
SIMANZI! MIILI YA MASISTA YAAGWA KABLA YA MISA TAKATIFU ST. THERESA WA AVILA BOKO