Arusha
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) inaendelea kishiriki katika mafunzo yenye lengo la kuimarisha usimamizi wa mikataba ya miradi ili kupunguza gharama na ucheleweshaji wa miradi.
Mafunzo hayo ya siku tano ambayo yamewaleta pamoja wadau muhimu katika Sekta ya Ujenzi wa Miundombinu ya barabara na usafirishaji pamoja na mambo mengine yanalenga kubadilishana uzoefu katika sekta hiyo muhimu kwa maendeleo ya kiuchumi na kijamii nchini.
Mkurugenzi wa Barabara kutoka TARURA, Mhandisi Venant Komba amewasilisha mada ya namna TARURA inavyo tekeleza majukumu yake, mikakati inayotumika katika usimamizi wa miradi, teknolojia zinazotumika katika ujenzi wa Barabara na changamoto zilizopo katika utekelezaji wa miradi hasa kipengele cha mikataba ikiwa ni sehemu ya kutoa uzoefu wa Wakala huo katika eneo hilo muhimu.
Akizungumza wakati wa uwasilishaji Mhandisi Komba amesema moja kati ya vipaumbele walivyonavyo kama taasisi ni kujengea wataalamu wao uwezo (capacity building) hasa katika maswala ya usimamizi wa mikataba ili kuepusha changamoto wakati wa utekelezaji wa miradi.
“Tunatumia nafasi kama hizi kama fursa ya kuendelea kujifunza kutoka kwa wenzetu’ amesema.
Mafunzo hayo yameandaliwa na Chama cha Barabara Tanzania (TARA) kwa kushirikiana Wahandisi washauri kutoka ndani na nje ya nchi.