Na Mwandishi Wetu- Mbalizi,Mbeya
Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) imetoa elimu kwa wananchi wa Wilaya ya Mbalizi kuchangamkia fursa za tenda za Serikali zinazotolewa kupitia Mfumo wa NeST, hususan kupitia upendeleo kwa Makundi Maalum ambao ni vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.
Akizungumza na wananchi hao waliounda vikundi kwa ajili ya shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii, Septemba 17, 2025 wilayani humo, Meneja wa PPRA Kanda ya Nyanda za Juu Kusini, Bw. Paschal Manono, alisema kanda hiyo imesajili Makundi Maalum 100 kwenye Mfumo wa NeST, ambayo yanaendelea kupata tenda za Serikali.
Alisema idadi hiyo bado ni ndogo ukilinganisha na wingi wa fursa zilizopo, kwani Sheria ya Ununuzi wa Umma inazitaka taasisi zote za Serikali kutenga asilimia 30 ya bajeti yake ya ununuzi kwa ajili ya Makundi Maalum.
“Zipo fursa za kipekee ambazo ninyi kama Makundi Maalum mnatakiwa kuzitumia. Sheria ya Ununuzi wa Umma kifungu cha 64 imeeleza wazi kuwa taasisi ambazo hazitatenga asilimia 30 ya bajeti yake ya ununuzi kwa ajili ya Makundi Maalum zitachukuliwa hatua. Hii ni nafasi yenu ya kushiriki na kufaidika,” alisema Manono.
Aliongeza kuwa kazi nyingine zinazoweza kufanywa na makundi hayo ni pamoja na upandaji miti, usafi wa mazingira, kazi za ukarabati mdogo wa barabara, ujenzi mdogo na uuzaji wa bidhaa kwa taasisi za umma. Michakato hiyo yote hufanyika kupitia Mfumo wa NeST.
“Makundi Maalum yanaweza kupata zabuni za hadi shilingi milioni mia tano, na hadi kufikia kikomo cha kuwa kundi maalum inapaswa kuwa yamepata zabuni za hadi shilingi bilioni tano,” Bw. Manono aliongeza.
Manono aliwahimiza viongozi wa vikundi kufika katika ofisi za PPRA zilizopo Jengo la NHIF ghorofa ya tano wanapohitaji huduma kuhusu Mfumo wa NeST na Sheria ya Ununuzi wa Umma; na wanaweza kuwasiliana kupitia namba ya huduma kwa wateja iliyotolewa na mamlaka hiyo.
Kwa upande wake, Shukran Thobias Mboma, Kiongozi wa Kikundi cha Vijana cha Mbombo – Mbalali, alisema mafunzo hayo ni yamewapa mwanga zaidi wa kuongeza njia za kujipatia kipato kwani awali waliamini tenda hutolewa kwa watu fulani wanaochaguliwa na Serikali. Hivyo, alisema wataendelea kuhamasishana na kupata elimu zaidi ili wakamilishe utaratibu wa kujisajili kwenye Mfumo wa NeST.