
Kada wa Chama Chama Cha Maponduzi na Mbunge wa zamani wa Jimbo la Moshi Vijijini, Thomas Ngawaiya jana amemuombea kura mgombea Ubunge wa Jimbo la Ubungo, profesa Kitila Mkumbo katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika kata ya Makurumla, Magomeni jijini Dar es Salaam.
Ngawaiya ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa umoja wa wazazi wa Mkoa wa Kilimanjaro alisema Wana ubungo wamepata bahati ya kumpata Profesa Kitila ambaye ni msomi wa chup kikuu cha Dar es Salaam na ni mtu anayependa maendeleo kwa watu wake
“Profesa Mkumbo ni mmoja wa watu walioandaa Dira ya Taifa ya mwaka 2025 mpaka 2050, hivyo mchagueni ili akayatekeleze waliyoyaandaa kwa maendeleo yetu,”alisema Ngawaiya.
Kiongozi huyo ambaye aliwahi kuwa mnadhimu ndani ya bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania, alisema profesa Kitila pia alikuwa ni mmoja wa wataalam waliotengeneza Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya kipindi hiki Cha Uchaguzi, hivyo kuwa rahisi kwake kuitekeleza. Aliongeza kwamba yeye ameamua kulisemea jimbo la Ubungo na kumuombea kura Profesa Mkumbo kwasababu ameishi ndani ya jimbo hilo kwa miaka 45 kwani anamakazi yake jimboni humo hivyo anafahamu matatizo yake ambayo Profesa Mkumbo anaweza kuyatatua chini ya CCM.
“Profesa Kitila bado ni waziri wa mipango na uwekezaji, hivyo ni rahisi yeye kuonana na rais wa nchi na kufikisha kwake matatizo yenu kuliko mpinzani, hivyo Oktoba 29 mpeni kura yeye, Rais Samia na diwani wa kata hii,” alisema Ngawaiya.
Alisema kwenye uchaguzi wa mwaka huu angalieni ubora wa mtu ambaye Jimbo la ubungo tunaye na ni profesa Kitila.
Katika mkutano huo Profesa Kitila aliomba kura na alimuombea pia kura Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hasssni na Diwani Kimwaga.