Na MWANDISHI WETU
Serikali kupitia Wizara ya Kilimo na Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imeendelea na utekelezaji wa miradi ya Umwagiliaji ambapo watu zaidi 4,650 wanatarajiwa kunufaika na miradi hiyo katika mikoa ya Dodoma, Mwanza na Shinyanga.
Lengo ni kuboresha maisha ya wakulima, kuongeza uzalishaji wa mazao na kuimarisha usalama wa chakula nchini. Katika mikoa ya Dodoma, Mwanza na Shinyanga pekee, zaidi ya wakulima 4,650 wananufaika moja kwa moja kupitia miradi hii, huku ekari 9,750 zikitarajiwa kumwagiliwa.
Mkurugenzi Mkuu wa NIRC, Raymond Mndolwa, amebainisha kwamba Serikali inaendelea kusimamia zaidi ya miradi 780 ya Umwagiliaji nchini yenye thamani ya takribani trilioni 1.2.
Amesema hatua hiyo inaongeza matumaini mapya kwa jamii zinazotegemea kilimo kama uti wa mgongo wa maisha yao.
“Hadi sasa miradi 126 iko chini ya wakandarasi. Aidha zaidi ya shilingi bilioni 492 zimetumika, huku miradi 30 ikiwa imekamilika kwa zaidi ya asilimia 80 na mingine 60 ikiwa imepiga hatua ya zaidi ya asilimia 50 ya utekelezaji.
“Miongoni mwa miradi hiyo ni ujenzi wa mabwawa ya Membe, Mahiga na Nyida ambayo yanatarajiwa kubadilisha maisha ya maelfu ya wakulima,”amesema.
Amesema katika mkoa wa Dodoma, mradi wa Bwawa la Membe na Skimu ya Umwagiliaji ya Membe unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 42.34. Bwawa hilo litahifadhi maji kwa ajili ya ekari 6,175 na kuwahudumia wakulima wapatao 1,500, huku skimu ya umwagiliaji yenye thamani ya shilingi bilioni 19.39 ikinufaisha wakulima 650 katika ekari 988.
“Nyumba zaidi 75 za wakulima vijana walionufaika na mradi wa Building a Better Tomorrow (BBT) zimeanza kujengwa kwa lengo la kuboresha maisha na makazi ya wanufaika hao,”amesema.
Akizungumzia mradi wa Nyida Shinyanga, Mndolwa ameeleza kuwa, miongoni mwa miradi inayotekelezwa ni ujenzi wa bwawa ambapo utekelezaji wake umekuwa suluhisho la tatizo la ukame lililodumu kwa muda mrefu.
“Mradi huu utahudumia wakulima wapatao 1,500 na kumwagilia ekari 1,235 na kupitia uwepo wake, wakulima sasa wanaweza kulima mara tatu kwa mwaka, wakiweka mkazo kwenye mazao ya mboga mboga na matunda, ameeleza Mndolwa.
Aidha mbali na mabwawa, Mndolwa amebainisha kuwa Serikali imeanzisha mpango wa kitaifa wa kuchimba visima zaidi ya 67,000 katika halmashauri 184 ndani ya miaka nane.
“Mpango huu unatarajiwa kuwanufaisha wakulima zaidi ya 100,000, kila mmoja akimwagilia wastani wa ekari 2.5. Visima hivyo vinachimbwa katika maeneo kame yasiyo na mabwawa ili kuondoa utegemezi wa mvua,”amesema.
Ameongeza kuwa kwa mwaka huu wa fedha, Tume inalenga kuchimba visima 1,300, ambapo 70 vitachimbwa na wakandarasi katika mikoa 16 ikiwemo Dodoma, Pwani, Tanga, Mara, Songwe, Singida, Manyara, Lindi, Mtwara, Kigoma, Geita, Morogoro, Simiyu, Ruvuma na Njombe.
Pia visima vilivyosalia vitachimbwa kwa kutumia mitambo mipya ya kisasa iliyonunuliwa na ambayo tayari imeanza kazi mkoani Tabora.
“Serikali inalenga kumwagilia ekari milioni 12.5 ifikapo mwaka 2030, kutoka ekari milioni 3 za sasa. Dhamira hii inaakisi ajenda ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuleta maendeleo jumuishi, shamba kwa shamba na familia kwa familia. Kupitia miradi ya Umwagiliaji, Tanzania inaweka msingi wa kilimo chenye tija, uhakika wa chakula na ustawi wa jamii,”amesema.
Kwa upande wake Mhandisi Umwagiliaji mkoa wa Mwanza Bw.Said Kambi, ameeleza kuwa mradi wa Bwawa la Mahiga umeondoa changamoto ya mafuriko ya mara kwa mara katika Kijiji cha Mahiga kilichopo wilayani Kwimba, ambapo mradi huo unatarajiwa kuwahudumia zaidi ya wakulima 1,000 katika ekari 1,235.
Amesema wakulima hao watavuna mara mbili kwa mwaka, hatua itakayoongeza kipato na usalama wa chakula kwa familia zao.
Naye,
Mhandisi Umwagiliaji mkoa wa Dodoma Mha. Osward Urassa, amesema katika mkoa wa Dodoma, mradi wa bwawa la Membe na skimu ya Umwagiliaji ya Membe unatekelezwa kwa gharama ya shilingi bilioni 42.34.
Akieleza juu ya utekelezaji wa mradi huko amesema bwawa hilo litahifadhi maji kumwagilia ekari 6,175 na kuwahudumia wakulima wapatao 1,500, huku skimu ya umwagiliaji yenye thamani ya shilingi bilioni 19.39 ikinufaisha wakulima 650 katika ekari 988.
“Kwa upande wa miradi ya Jenga Kesho Iliyo Bora (BBT), kwa mkoa huu NIRC tunaendelea na utekelezaji wa miradi hiyo ujenzi wa nyumba 46 za Vijana na mbili za wafanyakazi ujenzi wa ofisi sehemu ya chakula zimekamilika kwa Chinangali na nyingine zinaendelea kwa Ndogowe huku uchimbaji wa visima shamba la BBT Chinangali visima 38 na visima 22 kwa mashamba BBT Ndogowe vimekamilika,lengo ni kuendelea kuimarisha Kilimo katika miradi hiyo,”amesema.
Baadhi ya wananchi ambao ni wanufaika na miradi hiyo akiwemo Ney Samweli, ambaye ni mkulima wa skimu ya Mahiga ameeleza kuwa manufaa yanayopatikana na miradi inayoendelea kutekelezwa ambayo ni miradi ya Mabwawa na uchimbaji wa visima ambapo mbali na shughuli za kilimo pia itaondoa adha ya mafuriko kwa kuwa mabwawa hayo yatatumika kuvuna maji na hivyo watakuwa na kilimo cha uhakika,kwa kuwa itaongeza tija katika kilimo kwa kuinua vipato vya wakulima.