Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita (RMO) Dkt. Omary Sukari akiwa katika picha ya pamoja na wataalamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) alipotembelea banda la taasisi hiyo leo lililopo katika Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini Geita kwaajili ya kuona huduma za upimaji na matibabu ya moyo zinazotolewa na wataalamu hao.
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita (RMO) Dkt. Omary Sukari akisaini kitabu cha wageni alipotembelea banda la Taasisi ya Moyo Jakaya Kiwkete (JKCI) lililopo katika Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojiaya Madini yanayofanyika katika viwanja vya Maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan Geita kwaajili ya kuona huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo zinazotolewa.
Afisa Masoko wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Agnes Mndasha akimweleza Mkemia Uchenjuaji wa dhahabu wa Chama cha Wachimbaji wa Madini Mkoa wa Geita (GEREMA) John Ngeda huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo wakati wa Maonesho ya Nane ya Kitaifa ya Teknolojia ya Madini yanayofanyika katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan mjini Geita. (Picha na JKCL)
Na Jeremia Ombelo – JKCI, Geita
Mganga Mkuu wa Mkoa wa Geita (RMO) Dkt. Omary Sukari ameipongeza Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kutoa huduma za kibingwa za uchunguzi na matibabu ya moyo kwa wananchi wa Mkoa wa Geita na mikoa ya jirani.
Pongezi hizo amezitoa leo alipotembelea banda la JKCI lililopo katika maonesho ya nane ya kitaifa ya teknolojia ya madini yanayofanyika katika viwanja vya Maonesho vya Dkt. Samia Suluhu Hassan vilivyopo mjini Geita.
Dkt. Sukari alisema ujio wa taasisi hiyo mkoani Geita ni fursa kwa wananchi ya kupata huduma za ubingwa bobezi za matibabu ya moyo pamoja na elimu ya kuweza kuepukana na magonjwa hayo ambayo yamekuwa tishio kwa jamii.
“Taasisi hii imekuwa msaada mkubwa kwetu, mara nyingi wamekuwa wakitupatia huduma hizi kupitia Hospitali ya Rufaa ya Kanda Chato (CZRRH) pamoja na maonesho haya ya madini kwa kipindi cha miaka mitatu mfululizo”, alisema Dkt. Sukari.
Kwa upande wa wananchi waliotembelea banda la Taasisi hiyo waliomba huduma hizo zitolewe mara kwa mara hata baada ya maonesho hayo kuamlizika ili kuwawezesha wananchi wanaoshindwa kufika kwenye maonesho hayo kupata huduma hizo wakati mwingine.
Justus Nkwabi mfanyakazi wa Geita Gold Mine (GGM) alisema kupitia maonesho hayo ameweza kuchunguza afya ya moyo wake katika misimu mitatu ambayo taasisi hiyo imetoa huduma katika maonesho ya madini na kupata ushauri ambao umemsaidia kulinda afya yake.
“Nimekuwa mfuatiliaji mzuri wa afya yangu tangu nilipoanza kufanya vipimo vya moyo mwaka 2023 kupitia Taasisi hii inavyoshiriki kwenye maonesho ya madini mara ya kwanza, kwakweli wananisaidia sana kila mwaka napata fursa ya kuchunguza afya yangu”, alisema Justus
Rajabu Shukuru mkazi wa Geita aliwashukuru wataalamu wa JKCI kwa kumpa elimu kuhusu magonjwa ya moyo kwani awali hakuwa na ufahamu wa kutosha kuhusu magonjwa hayo na namna ya kujikinga asiyapate.
“Nawashukuru sana wataalamu hawa wa JKCI, wamenifikia muda muafaka na kuniwezesha kufanya uchunguzi wa afya yangu, nimepata majibu mazuri kuwa moyo wangu uko salama, naomba na wananchi wengine waje wapate huduma hizi katika banda hili”, alisema Rajabu.