Na Mwandishi Wetu- Kondoa, Dodoma
Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora itaendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi katika kulinda haki za binadamu na utawala bora.
Kauli hiyo imetolewa Septemba 23, 2025 na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) Mhe.Mathew Mwaimu wakati akifungua mafunzo kwa Maafisa wa Jeshi la Polisi Wilaya ya Kondoa, Mkoa wa Dodoma
Mhe.Mwaimu amesema kuwa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora imekuwa ikishirikiana na Jeshi la Polisi katika utoaji wa elimu juu ya haki za binadamu na misingi ya utawala bora.
‘’ushirikiano huu pia tunaupata pindi THBUB inapotembelea vituo vya polisi na kuzungumza na maabusu’’ amesema Mhe.Mwaimu
Aidha, Mhe.Mwaimu ameongeza kuwa katika kipindi hiki cha mchakato wa uchaguzi, THBUB imejikita katika utoaji wa elimu kuhusu haki za binadamu na wajibu wa jeshi la polisi katika uchaguzi Mkuu
“ lengo la elimu hii ni kukumbusha juu ya masuala ya haki za binadamu wakati wa utekelezaji wa majukumu katika kipindi hiki cha uchaguzi” amesema Mhe. Mwaimu
Kwa upande wake Mratibu Mwandamizi wa Polisi Wilaya ya Kondoa, Bw. Desdeli Rugimbana ametoa pongezi kwa THBUB kwa kutoa mafunzo hayo kwa Askari Polisi na kusema kuwa yatasaidia kuwakumbusha kutekekeza majukumu kwa kuzingatia haki za binadamu.