Mkuu wa mkoa wa Rukwa Makongoro Nyerere wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake.
……………
Neema Mtuka
Sumbawanga
Rukwa :Wananchi wa mkoa wa Rukwa wamesema ujio wa Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni fursa kubwa ya kiuchumi, hususan kwa wafanyabiashara wadogo na sekta ya usafirishaji.
Wakizungumz leo Septemba 26 ,2025 baadhi ya wafanyabiashara wa vyakula na watoa huduma za usafiri akiwemo Sophia Katunka amesema Mwenge wa Uhuru utaongeza mzunguko wa fedha na kuongeza kipato chao kutokana na wingi wa watu watakaoshiriki katika mbio hizo.
“Ni fursa kwetu ,mwenge wa uhuru utakesha hapa manispaa ya Sumbawanga wananchi watakula na kunywa kwa hivyo tutafanya biashara ya chakulana kujifunza fursa nyingine kutokana na miradi itakayozinduliwa” amesema katunka.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Charles Makongoro Nyerere, amesema Mwenge wa Uhuru utawasili mkoani humo Septemba 28 katika Kijiji cha Kizi, Kata ya Paramawe, katika mji wa Namanyere, halmashauri ya Wilaya ya Nkasi.
Amefafanua kuwa Mwenge wa Uhuru utakimbizwa umbali wa kilomita 653.1 na unatarajiwa kuzindua jumla ya miradi 34 yenye thamani ya shilingi bilioni 55.3.
Kati ya miradi hiyo, miradi 7 itazinduliwa rasmi, miradi 15 itawekewa mawe ya msingi, huku miradi 12 ikitarajiwa kukaguliwa.
“Niwaombe wananchi ushirikiano mnaouonyesha katika mapokezi ya viongozi ndio tuonyeshe katika mapokezi ya mwenge wa uhuru”amesema Makongoro.
Sambamba na hilo pia mkuu huyo wa mkoa ametumia fursa hiyo kutangaza ujio wa mgombea urais kupitia chama cha mapinduzi (CCM) Dkt Samia Suluhu Hassan hapo oktoba 18 mwaka huu ambapo atazungumza na wananchi na kunadi sera za chama hicho.