NA.Sophia Kingimali.
WAKAZI wa Zanzibar wametakiwa kujitokeza kwa wingi kuchangamkia fursa iliyotolewa na chuo cha VETA FURAHIKA kwa wazazi kuwapeleke watoto wao chuoni hapo ili wapate elimu bure itakayowafaa katika maisha yao na kuwaondoa katika hatari ya kujiunga katika makundo ovu ya uasherati.
Dkt. David Msuya ambaye ni Mkuu wa Chuo Cha Ufundi Furahika jijini Dar es Salaam ametoa wito huo leo, Septemba 26, 2025 wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake na kubainisha kwamba masomo katika chuo hicho ambacho kipo Kituo cha Darajani Zanzibar yataanza Oktoba 20, 2025 na udahili wa wanafunzi ukitaraji kuanza wiki ijayo.
“Tumefungua Chuo Cha Ufundi pale Kituo Cha Darajani ghorofa ya pili na kozi zitazofundishwa kwa wanafunzi wa dini zote ni Makeup, Information Communication and Technology (ICT), English Language, French, Secretarial, Tourism, Event Planning Management, Food and Baverage Services zitafundishwa bure kwa vijana wote waliomaliza kidato cha nne na darasa la saba na kushindwa kuendelea na masomo kwa sababu mbalimbali,” amesema.
Ameongeza kuwa lengo la kutoa elimu bure ni kuunga mkono Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inayoongozwa na Rais Dkt Hussein Alli Mwinyi katika jitihada zake za kuwakwamua na kuwaendeleza vijana katika elimu ya kujitegemea ili waondokane na utegemezi.
Dkt Msuya alifafanua kuwa awali wanafunzi hao kutoka Zanzibar walikuwa wanakwenda katika Chuo Cha Furahika Dar es Salaam kusoma fani mbalimbali na mwaka jana wanafunzi 400 walihitimu mafunzo katika kazi ikiwemo Hoteli, umeme wa magari, Makeup, ufundi nguo na nyinginezo.
Amesema kutoka na kuwepo kwa gharama kubwa za malazi na chakula kwa wanafunzi hao, ndipo wakaamua kufungua chuo Zanzibar ili kupunguza hadha na sasa wahitaji wanaweza kujiunga na chuo kilichopo Darajani.
Chuo cha Furahika Islamic Vocatinal Centre chenye usajili namba VTC/PRP/2025/0001/01 ikiwa ni moja ya tawi la Chuo cha Furahika Dar es Salaam.
Sambamba na hayo uongozi wa Chuo cha Ufundi Stadi Furahika kinachopatikana Buguruni Malapa jijini Dar es Salaam kimetoa salamu za pole kwa familia ya Rais wa Serikali Mapinduzi Zanzibar kutokana na kifo cha Abbas Mwinyi, ambaye ni kaka wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt Hussein Alli Mwinyi .
Abbas, ambaye pia ni mtoto wa marehemu Rais mstaafu Alli Hassan Mwinyi, alikuwa mgombea ubunge kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika Jimbo la Fuoni, Zanzibar alifariki dunia jana katika Hospitali ya Lumumba mjini Unguja na amezikwa leo katika eneo la Bweleo na kuhudhuriwa viongozi mbalimbali visiwani humo.
“Sisi Chuo cha Furahika kwa masikitiko makubwa tunatoa pole kwa Rais wa Zanzibar na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Dkt Hussein Alli Mwinyi na familia kwa ujumla kwa kuondokea na kaka yao, hivyo tunamuomba Mungu ampe nguvu katika kipindi hiki kigumu na ailaze roho ya marehemu Abbas, mahala pema peponi ,” amesema.
Marehemu Abbas kabla ya umati, alikuwa mgombea aliyeteuliwa na CCM kuwania ubunge katika Jimbo la Fuoni, ingawa awali alikuwa mbunge wa jimbo hilo tangu mwaka 2015 na katika uchaguzi wa mwaka huu alikuwa anatetea kiti hicho.