Na Mwandishi wetu, Ngorongoro
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro kwa kushirikiana na wadau wa utalii imefanya maadhimisho ya siku ya utalii duniani kwa kuhamasisha utalii wa kupanda milima kupitia mlima Lolmalasin leo tarehe 27 Septemba, 2025.
Mlima huo unaotajwa kuwa ni wa tatu kwa urefu Tanzania ukiwa na urefu wa mita 3,682 kutoka usawa bahari , ni moja Kati ya mazao ya utalii yanayopatikana ndani ya Eneo la Ngorongoro ambao umekuwa ukiwavutia watalii wengi hasa wale wanaopenda kupanda milima kutokana na mandhari yake nzuri ya Asili.
Akizungumza wakati wa kupanda mlima huo, Kamishina Msaidizi Mwandamizi anayesimamia Huduma za Utalii na Masoko NCAA Mariam Kobelo amesema kwamba maadhimisho haya yanalenga kuhamasisha utalii kupitia mazao mbalimbali ya utalii yaliyopo ndani ya eneo la hifadhi ya Ngorongoro.
“Leo tunapoadhimisha siku ya utalii duniani tunatumia fursa hii kutangaza mlima Lomalasin na kuhamasisha watalii wa ndani kuja kufanya matembezi ya mlimani katika mlima huu” alisema Kobelo
Kwa upande wake Mdau wa utalii ambaye ni Mkurugenzi wa kampuni ya utalii ya Land Afrika Safaris Bw. Timothy Mdinka amesema kwamba pamoja na kuwa na mandhari nzuri mlima huo upo kwenye eneo lenye jiologia ya pekee inayoinganisha Afrika kwa namna ya Kipekee zaidi.
“ Mlima huu kwetu sisi ni mlima wa pekee sana ambao unakuwa ukiwavutia wageni wengi kutoka na jiografia yake ambayo imepakana na vivutio vingine vya utalii ikiwemo kreta ya empakai, Kreta ya Olmoti, Mlima Losirwa, Oldoinyo Lengai na Engaruka” Alisema Timoth
Siku ya utalii duniani huadhimishwa kila mwaka septemba 27, ikiwa na lengo la kuhamasisha maendeleo ya utalii endelevu na kuongeza uelewa wa jamii kuhusu mchango wa utalii katika maendeleo ya kiuchumi, kijamii na kiutamaduni ambapo kwa mwaka huu kauli mbiu ni “Utalii na mageuzi endelevu”.
Maadhimisho haya yameudhuriwa na wadau mbalimbali wa utalii wakiwemo Wizara ya Maliasili na utalii, Halmashauri ya Wilaya ya karatu, Land Africa Safaris, Azam Tv, Crater Lodge, Asante tours, Nols , & Beyond pamoja na wenyeji wa Kijiji cha Bulati unakopatikana Mlima Lomalasin.