NA JOHN BUKUKU- PWANI
Mgombea Urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Samia Suluhu Hassan, ameendelea na kampeni za chama hicho Septemba 28, 2025, mjini Kibaha mkoani Pwani.
Akizungumza na wakazi na wananchi wa Pwani, amesema kuwa Serikali inaendelea kutekeleza mradi mkubwa wa mtandao wa gesi kutoka Kinyerezi hadi Mkoa wa Pwani, lengo likiwa ni kuhakikisha viwanda vinapata nishati ya uhakika kwa maendeleo ya uchumi na ustawi wa wananchi.
Dkt. Samia amesema mtandao huo wa gesi utasaidia kupunguza gharama za uzalishaji viwandani, kuongeza ushindani wa bidhaa za ndani, na kuleta unafuu wa maisha kwa wananchi wa kawaida wanaotegemea huduma za viwanda hivyo. Amefafanua kuwa gesi hiyo pia itatumika majumbani na katika shughuli za kibiashara, hatua itakayopunguza matumizi ya kuni na mkaa na hivyo kulinda mazingira.
Aidha, ameeleza kuwa mradi huo ni sehemu ya mikakati ya muda mrefu ya Serikali kuhakikisha Mkoa wa Pwani unakuwa kitovu cha viwanda na nishati, ambapo gesi hiyo itakuwa chachu ya uwekezaji mkubwa wa viwanda vipya na kuimarisha upatikanaji wa ajira kwa vijana.
Ameongeza kuwa Serikali itaendelea kushirikiana na sekta binafsi kuhakikisha mradi huo unakamilika kwa wakati na unaleta manufaa ya moja kwa moja kwa wananchi wa Pwani na Watanzania kwa ujumla.
Aidha, ameeleza kuwa Mkoa wa Pwani umeendelea kushuhudia ukuaji mkubwa wa viwanda, ambapo zaidi ya viwanda 287 vimejengwa, vikiwemo vikubwa na vidogo, na kutoa ajira za moja kwa moja 21,049 na zisizo za moja kwa moja 960,000.