Kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa Ismail Ali Ussi wakati akiweka jiwe la msingi ujenzi wa daraja katika kata ya Isunta wilayani Nkasi
Katikati ni kiongozi wa mbio za Mwenge wa uhuru kitaifa Ismail Ali Ussi wakati akikagua daraja la upinde wa mawe wilayani Nkasi
Rosemary Malaji mkazi wa Isunta wakati akizungumzia adha waliyoipata kabla ya ujenzi wa daraja la upinde wa mawe wilayani Nkasi
Ernest Hagai mkazi wa Namanyere akizungumza kuhusu kukamilika kwa daraja la upinde wa mawe.
………..
Na Neema Mtuka Nkasi
Rukwa: Wananchi kata za Isunta na Namanyere Halmashauri ya Wilaya ya Nkasi mkoani Rukwa wameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa hatua ya kuendelea kuboresha miundombinu ya barabara, hatua ambayo imetatua kero ya muda mrefu katika eneo hilo.
Wakizungumza leo Septemba 28,2025 wananchi hao akiwemo Rosemarry Malaji amesema kabla ya maboresho hayo walikabiliwa na changamoto kubwa zilizochangia hata kupoteza maisha ya watu kutokana na ugumu wa kupita katika maeneo hayo.
“Tulikuwa tunalazimika kuzunguka makaburi kwa kuwa kivuko hicho kilikuwa hatarishi kwani watu wengi wamepoteza maisha hasa kipindi cha masika ambapo mto huo hujaa maji”.amesema Malaji
Aidha, wameeleza kuwa ujenzi wa daraja jipya utafungua ukurasa mpya wa mawasiliano, kwani sasa utarahisisha usafiri na usafirishaji sambamba na huduma muhimu kufikishwa kwa urahisi kwa wakazi wa kata hizo na maeneo ya jirani.
Ernest Hagai mkazi wa Namanyere amesema kuwa aliwahi kushuhudia mwanafunzi akisombwa na maji kipindi cha nyuma kwa hivyo daraja hili litapunguza changamoto hiyo.
“Ilikuwa ni kipindi cha masika ambapo wanafunzi wanavuka kwenda shule nilishuhudia mwanafunzi akisombwa na maji kwa kweli kivuko hiki kilikuwa hatarishi sana kwa maisha ya watu”amesema Hagai
Akizungumza wakati akiweka jiwe la msingi katika ujenzi huo, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ali Ussi, amewataka wananchi kuendelea kuiunga mkono Serikali kwa kuilinda na kuitunza miundombinu hiyo muhimu ili iwe na manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
“Kivuko hiki ni fursa kwenu wananchi kwani kukamilika kwake kutawapa fursa ya mawasiliano,kusafirisha mazao na kupata huduma za usafiri wa uhakika wakati wote.” Amesema Ussi.