*Agusia ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Tanga ,Moshi ,Arusha hadi Musoma
Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Kilimanjaro
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema Serikali iko mbioni kukamilisha mazungumzo kuanza utekelezaji wa mradi wa Liganga na Mchuchuma ambao unahusisha uchimbaji wa madini ya chuma na makaa ya mawe.
Akizungumza leo Oktoba 1,2025 mbele ya maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Arusha akiendelea na mikutano ya kampeni kuelekea uchaguzi mkuu Oktoba 29 mwaka huu amesema hilo analisma kwa uhakika kwa sababu tayari Serikali ipo kwenye mazungumzo.
“Serikali ipo katika mazungumzo ya mwisho kabisa kuanza kazi kwenye mgodi wa Mchuchuma na Liganga mgodi wenye chuma nyingi sana na makaa ya mawe mengi sana.
“Tupo katika hatua za mwisho mgodi ule ndiyo utakaolisha viwanda vingine kama cha Kilimanjaro Tools. Miradi mingine ya kimkakati itakayochochea uchumi wetu ni ujenzi wa reli ya kisasa kutoka Tanga hadi Musoma,” amesema.
Kwa upande wa viwanda Dk.Samia amesema awali mji wa Moshi ulikuwa na viwanda vingi vya kimkakati ambavyo baada ya ubinafsishaji viwanda vingi vilishindwa kuendelea.
Hivyo amesema kwamba itahakikisha viwanda vinafanyakazi kwa kuwatafuta waendeshaji wengine ikiwemo vyama vya ushirika.
Amesema kwa Moshi Serikali imefufua kiwanda cha Kilimanjaro Machine Tools kilichosimama kwa zaidi ya miaka 30 ambapo tayari kinatoa huduma kutengeneza vifaa kwa ajili ya viwanda.
“Mkitupa ridhaa tutakiimarisha kiwanda hiki kwa kuhakikisha kinapata malighafi ya chuma ya kutosha pamoja na makaa ya mawe kuinua uchumi wa mkoa wetu.
Ameongeza kwamba hivyo reli hiyo itapita Moshi na Arusha ambapo mradi huo utakuja na fursa za ajira kwa wananchi kuchochea zaidi biashara na uchumi katika ukanda wa kaskazini.
Wakati huohuo Dk.Samia amezungumzia kuhusu upatikanaji maji, amesema katika Wilaya ya Hai serikali imekamilisha mradi wa maji kutoka Uroki – Bomang’ombe – Kikafu kwa gharama ya sh. bilioni 3.3.
Kwa upande wa Rombo, amesema Serikali inatekeleza mradi wa sh. bilioni 9.8 kutoa maji Ziwa Chala kwenda Rombo.
“Tutatumia maeneo yenye maji mserereko kupeleka maji kwa wananchi ikiwemo maeneo ya Ringai na Marangu.
Kuhusu wilayani Siha, amesema kwamba kuwa Serikali inatekeleza mradi wa sh. bilioni 14 kupeleka maji vijiji nane.
Katika hatua nyingine Dk.Samia amesema katika elimu pia serikali itajenga kampasi ya Chuo cha Biashara(CBE) wilayani Hai ambacho kitaleta karibu fursa ya mafunzo ya elimu na kuimarisha uchumi wa eneo hilo.