Na mwandishi wetu
Naibu Kamishna wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro anayesimamia Uhifadhi,Utalii na Maendeleo ya Jamii Joas Makwati Oktoba 1 mwaka 2025 ameongoza kikao cha ujirani mwema na viongozi wa maeneo ya vijiji vya jirani na kusisitiza umuhimu wa ushirikiano ili kujenga mazingira mazuri ya kufanya kazi pamoja.
Katika kikao hicho pamoja na watendaji wengine Naibu Kamishna aliongozana na Kamishna Msaidizi Mwandamizi anayeshughulikia maendeleo ya jamii Bi. Gloria Bideberi ambapo viongozi wote walikubaliana kufanya kazi kwa pamoja.
Viongozi wa vijiji wa wilaya ya Karatu na Monduli walieleza changamoto kubwa zinazowakabili wananchi, ikiwemo kupoteza mazao kutokana na uvamizi wa wanyama pori kama tembo na nyati wanaoingia katika makazi na mashamba, hali inayohatarisha shughuli za kiuchumi za kaya nyingi zinazotegemea kilimo.
Naibu Kamishna Joas Makwati alieleza kuwa pamoja na suala zima la ujirani mwema kikao hicho kitasaidia kuweka mikakati ya pamoja katika kutatua changamoto baina ya binadamu na wanyama pori wakali na waharibifu.
Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro inaendelea na ziara za kukutana na wananchi katika vijiji mbalimbali ili kuimarisha ujirani mwema.