Dar es Salaam
Wakala ya Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) kupitia mradi wa RISE umefanikiwa kutekeleza kipengele cha uondoaji vikwazo katika barabara (bottleneck) kwa kurejesha mawasiliano ya barabara zenye urefu wa Kilomita 2227 ambazo zimeweza kuhudumia wananchi wapatao 2,690,000 waliopo katika kata 263 na vijiji 762 katika maeneo mbalimbali nchini.
Hayo yamesemwa na Mhandisi wa TARURA kutoka mradi wa RISE, Ephraim Kalunde wakati wa kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Wahandisi yaliyofanyika mwishoni mwa wiki katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es Salaam.
“Mpaka sasa utekelezaji umefikia asilimia 95, tumejenga vivuko katika halmashauri za wilaya 130 katika mikoa 25 ya Tanzania Bara isipokuwa mkoa wa Dar es Salaam na tunategemea mpaka kufikia mwishoni mwa mwezi Oktoba tutakuwa tumekamilisha ujenzi wa vivuko hivyo na wananchi wataweza kupita katika maeneo yaliyokuwa yakisumbua na korofi ili kuzifikia huduma za kijamii”, amesema.
Mhandisi Kalunde ameeleza kuwa mradi wa RISE pia unatekeleza ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami Kilomita 400 katika halmashauri za Iringa, Kilolo, Mufindi, Mbogwe, Handeni na Ruangwa ambapo awamu ya kwanza zimejengwa Kilomita 33 na Kilomita 367 zilizobaki zipo katika taratibu za manunuzi ili kumpata mkandarasi.
Ameongeza kuwa kupitia mradi wa RISE pia kuna kipengele cha matengenezo madogo madogo ya barabara kwa kutumia vikundi (nguvukazi), nguvukazi hizo ni wale wananchi wanaoishi karibu na maeneo ya barabara wenye uwezo wa kufanya shughuli za matengenezo ya barabara umbali usiozidi Kilomita 5 kutokea kwenye makazi yao.
“Vikundi hivi vimepatiwa mafunzo na vyeti na sasa watajisajili kama wakandarasi wadogo wadogo ambao watafanya kazi za kusafisha alama za barabarani zilizofutika, kukata nyasi na kusafisha mifereji. Watafanya kazi hizi katika vipindi maalum kipindi cha mvua na jua kali. Hii itasaidia taasisi yetu kupunguza gharama za matengenezo ya barabara”, amesema.
Mradi wa RISE ni mradi unaogharamiwa na mkopo nafuu toka Benki ya Dunia ambapo unatekelezwa katika kipindi cha miaka 6, mradi umeanza Novemba 2021 na unatarajiwa kukamilika ifikapo Juni 2027 ambapo mpaka sasa mradi upo zaidi ya asilimia 60 ya utekelezaji.