
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) limeeleza kuwa kumetokea changamoto ya manunuzi ya umeme (LUKU) hali inayosababisha Wateja wake kushindwa kununua umeme kupitia njia za mitandao ya simu, Mawakala pamoja na njia za kibenki.
Katika taarifa yake kwa Umma, TANESCO imesema kupitia Wataalamu wake imejiridhisha kuwa changamoto hii inasababishwa na hitilafu kwenye mfumo wa malipo ya Serikali (GePG) ambapo tayari Wataalamu wa mfumo huo wanashughulikia changamoto iliyojitokeza ili huduma iweze kurejea katika hali ya kawaida.
“TANESCO inatoa wito kwa Wataalamu wa GePG kushughulikia jambo hili kwa umuhimu mkubwa ili kuwaondolea Wateja usumbufu wa kushindwa kufanya manunuzi ya umeme kunakosababishwa na changamoto hiyo, Shirika litawafahamisha Wateja wake huduma zitakaporejea kikamilifu”