
……
Happy Lazaro, Arusha
Arusha .Maboresho ya mfumo wa utoaji na usimamizi wa leseni za madini yanatajwa kupunguza urasimu na kurahisisha upatikanaji wa leseni kwa wachimbaji na wawekezaji kwa haraka zaidi, tofauti na ilivyokuwa awali.
Kutokana na maboresho hayo, Tume ya Madini imeandaa mafunzo maalum kwa maafisa wa madini wanaoshughulikia leseni kutoka mikoa yote ya kimadini nchini, ili kuwaongezea uelewa na kuwajengea uwezo katika uchakataji wa maombi ya leseni.
Akifungua mafunzo hayo jijini Arusha kwa niaba ya Katibu Mtendaji wa Tume ya Madini, Mkurugenzi wa Huduma za Sheria, Francis Kayichile, amesema maboresho yaliyofanyika yanalenga kuhakikisha muda wa kupata leseni unapungua, endapo mwombaji atakuwa ametimiza masharti yote kwa mujibu wa sheria.
“Tumeona ni vyema kuwakutanisha maofisa leseni kutoka mikoa zaidi ya 30 ya kimadini ili tuweze kujadili na kubadilishana uzoefu kuhusu maboresho ya mfumo huu. Lengo ni kumrahisishia Mtanzania au mwekezaji anayehitaji leseni, bila kukumbana na urasimu,” amesema.
Ameongeza kuwa maboresho hayo pia yanakusudia kufunga mianya ya upotoshaji na matumizi mabaya ya nafasi, ambapo mifumo ya TEHAMA inatarajiwa kusaidia kudhibiti changamoto hizo.
Kwa mujibu wa Kayichile, washiriki wa mafunzo hayo wanatarajiwa kujifunza na kujadili masuala mbalimbali kuhusu maboresho ya mfumo huo pamoja na taratibu sahihi za uchakataji wa maombi ya leseni kwa mujibu wa Sheria ya Madini, Sura ya 123 na kanuni zake.
“Nitumie nafasi hii kuwakumbusha kutumia muda huu wa mafunzo kujadili na kuweka mikakati ya kusafisha taarifa za leseni katika mfumo (data cleaning) ili tuwe na taarifa sahihi,” ameongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Leseni kutoka Tume ya Madini, Mhandisi Aziza Swedi, amesema Tume imeona umuhimu wa kukutana na maafisa hao ili kujadili changamoto zinazojitokeza wakati wa uchakataji wa leseni na kuzitafutia ufumbuzi wa pamoja.
Amesema baada ya maboresho ya mfumo huo, Tume imekuwa ikiendesha mafunzo ya mara kwa mara ili kuongeza ufanisi na kuboresha huduma kwa wawekezaji.
“Kila maboresho huambatana na changamoto katika utekelezaji. Hivyo tuliona ni vyema kukutana na maafisa hawa ili kutatua changamoto hizo pamoja, na hatimaye kuboresha huduma kwa wachimbaji na wawekezaji,” amesema.
Mhandisi Swedi ameongeza kuwa maboresho hayo yamechangia ongezeko la mapato, ambapo katika mwaka wa fedha 2024/2025 Wizara ya Madini ilipangiwa kukusanya Shilingi bilioni 999, lakini ilifanikiwa kuvuka lengo na kukusanya zaidi ya Shilingi trilioni 1.07.
Naye Mjiolojia kutoka mkoa wa Songwe, George Mchiwa, amesema mfumo mpya umeondoa changamoto nyingi zilizokuwepo awali na umeboresha upatikanaji wa leseni kwa wakati.
“Mafunzo haya yatasaidia zaidi kuongeza ufanisi, kutukumbusha wajibu wetu, na kuhakikisha tunaendana na taratibu na sheria zilizopo,” amesema.
Afisa Leseni mmoja aliyehudhuria mafunzo hayo amesema utoaji wa leseni kwa sasa unaendelea vizuri, huku elimu ikiendelea kutolewa kwa wachimbaji na wawekezaji juu ya umuhimu wa kuwa na leseni, jambo linalosaidia kuongeza pato la serikali na kudhibiti uchimbaji holela.