Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Arusha
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi(CCM)Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema Serikali itaendelea kuweka msisitizo kuimarisha sekta za madini.
Amesema Serikali katika miaka mitano iliyopita walijiwekea lengo la kufikia asilimia 10 ifikapo 2025 huku mchango wa madini kwenye pato la taifa umeongezeka kutoka asilimia 6.8 mwaka 2020 hadi asilimia 10 mwaka 2024.
Akizumgumza wakati wa mkutano wa kampeni kwa ajili ya kuomba kura kuelekea Oktoba 29 mwaka huu,Dk.Samia amewaambia wakazi wa Mkoa wq Arusha serikali ilifikia lengo kabla ya kufika 2025.
“Niwajulishe kwamba lengo lilolofikiwa ni asilimia 10.1 ya pato la taifa kwa mwaka jana ikiwa ni mwaka mmoja kabla ya kipindi tulichojiwekea. Tumeanza kuyatumia madini kuimarisha uwezo wetu wa kujitegemea kiuchumi.
“Tumeanza kuweka akiba yetu ya dhahabu ndani ya benki kuu na akiba imekuwa ikikua mwezi hadi mwezi na ndiyo maana shilingi ya Tanzania imeendelea kuwa madhubuti.”
Pia, amesema Serikali imechukua hatua kuhakikisha Tanzania inanufaika zaidi kupitia madini ya Tanzanite kwa kuweka kituo cha uuzaji Pamoja wa madini hayo eneo la Merarani.
Vilevile, amesema Serikali imeanzisha minada ya vito ambapo mnada wa kwanza ulifanyika Mirerani na mnada wa pili ulifanyika mkoani Arusha ambayo imeitangaza vyema Tanzania katika biashara ya vito.
Hivyo amesema akipewa ridhaa ya kuliongoza taifa, Serikali yake itahamasisha zaidi shughuli za uongezaji thamani madini ili manufaa Zaidi yapatikane ikiwemo ajira kwa vijana.
Pia amesema kupitia kituo cha jiolojia Tanzania serikali itaongeza kasi ya utoaji mafunzo kuhusu uongezaji thamani madini kwa viwango vinavyokubalika kimataifa.
“Nchi yetu tumepima madine yote yanayochimbwa nchi nzima ni asilimia 16 ndiyo imepimwa, tuna lengo miaka mitano ijayo kupima tena asilimia 18 hadi 20 ya nchi kubaini madini tuliyonayo wapi yapo…
“Na tuwaalike wataalamu waje tuone namna ya kuchimba madini hayo ili kukuza ajira kwa vijana.Mwelekeo na kipaumbele chetu ni wachimbaji wadogo.”
Kuhusu mashamba ya Kili Flora amesemamashamba hayo matano Kili Flora Usa River, Arusha Blooms, Kili Flora na Nduruma ni kwamba mashamba hayo wawekezaji wameshindwa kuyanedeleza.
“Tulichofanya tumeunda timu ya makatibu wakuu wamekwenda kuyafanyia tathmini ili serikali ikae na wawekezaji tuelewane mashamba yake yachukuliwe na serikali.
“Na baadhi ya mashamba tutakaa na uongozi wa mkoa kuangalia uwezekano wa serikali kuyaendeleza kuyawekea miundimbinu tuyaingine kwenye mtindo wa BBT kwa vijana.”
“Tutaangalia mazao gani vijana wetu wanaweza wakalima kwenye mashamba yale. Lakini shamba lingine sehemu ya shamba tunakwenda kufanya kilimo cha mjini. Eneo lingine tunakwenda kupima kwa ajili ya makazi ya watu. Arusha inakuwa Arusha ni jiji lazima litanue maeneo yake,” alisisitiza.
Ametumia nafasi hiyo kuuomba uongozi wa mkoa kuhakikisha mashamba hayo hayaharibiwi kwani baadhi ya wananchi wameshaanza kufanya uvamizi hivyo alisisitiza mashamba hayo yatakuja kuendelezwa kwa ajili ya vijana.
Wakati huo huo akiomba kura kwa wakazi wa Mkoa wa Arusha Dk.Samia amesema Serikali kwa awamu zote imeweza na wakirudishwa kuongoza nchi wataweza .
“Tupeni ridhaa tena tutaweza tuna kila njia ya kufanya tuweze, tuna kila mbinu, tuna kila fursa ya kuitumia na kufanya tuweze kutekeleza yale tuliyoyaweka kwenye Ilani.”