*Azungumzia mashamba yasiyoendelezwa… Shamba la Basutu utaratibu ni ule ule
Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Manyara
MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan amesema mkakati wa Serikali katika miaka mitano ijayo ni kuiwezesha Wilaya ya Hanang mkoani Manyara iweze kuzalisha tani milioni moja ya ngano ifikapo mwaka 2030.
Akizungumza leo Oktoba 3,2025 wilayani Hanang mkoani Manyara akiendelea na mikitano ya kampeni kuomba kura Dk.Samia amesema Serikali inafahamu wakazi wa Hanang ni wakulima wazuri wa ngano.
“Najua ngano na mazao mengine kama mbaazi, dengu na mazao mengine niwaahidi tutaendelea kuwaletea pembejeo za kilimo.
“Lengo letu kitaifa kufikisha tani milioni moja ifikapo 2030 kutoka Hanang ili tuweze kujitegemea kwa mahitaji ya ngano. Kilimo kikubwa huku ni ngano kwa hiyo tunataka Hanang ituzalishie ngano tani milioni moja itakapofika 2030.
Ameeleza hatua zitakazochukuliwa ni kushughulikia mashamba makubwa ambayo yalitolewa kwa wawekezaji ambao hawajayaendeleza.
Dk. Samia ameitaka Mamlaka ya Maeneo Huru ya Uwekezaji waangalie upya mikataba ya uwekezaji na namna yatakavyoweza kurudishwa mashamba hayo huku akifafanua hatua hiyo itawezesha mashamba hayo kugawanywa kwa wakulima kisha kuzalisha mazao.
“Haipendezi kwamba tuna mashamba ambayo yanaweza kuzalisha ngano nyingi lakini tunaagiza ngano nyingi kutoka nje huku mashamba yamekaa bila kuzalisha.
“Tunakwenda kuyaangalia mashamba hayo. Tumeitaka mamlaka ya maeneo huru ya uwekezaji kuangalia jinsi tunavyoweza kuyachukua.
Kuhusu shamba la Basotu amesema Serikali imeamua kuendelea na utaratibu uliopo kuwa chini ya msajiri wa hazina huku halmashauri ya Hanang iendelee kuyasimamia wakati mwekezaji akisubiriwa.
Ametoa mwito kwa wananchi kuendelea kulitumia shamba hilo kwa gharama nafuu huku akiiagiza halmashauri kuweka gharama hizo wazi ili wakulima wazifahamu.
“Kwa sababu tumegundua kuna mambo mambo huko ndani, wakulima wanataka maeneo ya kulima lakini halmashauri mna mambo yenu. Kwa hiyo tunataka gharama ziwekwe wazi ili tuepushe vishoka katika shamba hilo.
Kuhusu bei ya mbaazi amesema wanunuzi wa kati nao wanasababu nyingi ya kutelemsha bei ambapo alisema serikali ipo katika majadiriano na India.
Amesema uzalishaji wa mbaazi duniani umeongezeka hivyo bidhaa inapokuwa nyingi sokoni bei inashuka.“Katika mazungumzo hayo hata kama bei imeshuka isiwe chini ya asilimia 70 ya msimu uliopita.
“Najua wanaotaka kushusha bei wana lawama nyingi kwa mfumo wa stakabadhi ghalani lakini mfumo huu huu bei zinapopanda mfumo huu unafanyakazi pia.
“Kushuka na kupanda kwa bei ni mambo ya biashara, mazao yakiwa mengi sokoni bei zinashuka tukivuna sisi wengine hali ya hewa haikuwapendelea bei zinapanda.”
Amewaeleza wakulima wa zao hilo kutovunjika moyo kwani serikali ina shughulikia suala hilo.Pia Serikali itaanzisha kilimo cha unwagiliaji kwa kujenga bwawa litakalokinga maji ya mvua ambayo yatatumika kwa kumwagilia.
Akizungumzia kuhusu mawasiliano ya simu alisema inajipanga kujenga minara mitano ya mawasiliano ya simu katika vijiji vya Sipai, Mogutu, Nalaji, Kisakala na Gidamula.Amesema ni muhimu kuwepo mtandao wa mawasiliano kwani simu ndiyo kila kitu.
Pamoja na hayo Dk.Samia amewaomba wananchi ifikapo Oktoba 29 mwaka huu waende kupiga kura.”Twendeni tukapige kura ,kwanini nina wahimiza kufanya hivyo .Nawahimiza hivyo mkimpiga mtu mchape kweli kweli, akumbuke kwamba nilichapwa.Twendeni tukapige kura kweli kweli CCM iweke heshima yake.”