Jeshi la Polisi nchini Tanzania kupitia kwa Msemaji wake DCP David Misime limesisitiza kuwa bado linaendelea kumsubiri Ndugu Humphrey Polepole ili aripoti katika Ofisi ya Mkurugenzi wa upelelezi wa Makosa ya jinai ili atoe maelezo kuhusu tuhuma mbalimbali alizozitoa kupitia Mitandao yake ya Kijamii.
Ikumbukwe kuwa Jumatatu Septemba 15, 2025 Jeshi la Polisi lilisema kuwa limefungua jalada la uchunguzi na linaendelea kuchunguza tuhuma mbalimbali ambazo amekuwa akizitoa kada huyo wa Chama Cha Mapinduzi CCM.
“Tuhuma ambazo ametoa na anaendelea kuzitoa kulingana na jinsi alivyozielezea zinaashiria uwepo wa makosa ya kijinai na kwa mujibu wa sheria zinahitaji ushahidi wa kuzithibitisha zitakapo wasilishwa mahakamani.
Tuhuma hizo amekuwa akizitoa kupitia mitandao ya kijamii, baada ya kufungua jalada na kuanza uchunguzi, Jeshi la Polisi mbali na kukusanya ushahidi, limekuwa likifanya jitihada za kumpata ili aweze kutoa maelezo au ushahidi na vielelezo vitakavyo thibitisha tuhuma hizo ili kuwezesha hatua zingine za kisheria ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria na ndivyo utaratibu wa kisheria ulivyo” Taarifa hiyo ya Polisi ilieleza.
Katika hatua nyingine Jeshi la Polisi limeeleza kuona taarifa zinazosambazwa kwenye Mitandao ya kijamii na ndugu zake kuwa Mtu huyo ametekwa usiku wa kuamkia Oktoba 06, 2025 na kueleza kuwa tayari wameanza kufanyia kazi taarifa husika ili kupata ukweli wa madai ya kutekwa kwake.