
“Leo hii, mkulima wa parachichi kijijini Madeke mkoani Njombe anaweza kupata huduma kupitia AMCOS yake inayotoa huduma za CRDB Wakala; mwalimu kutoka wilaya ya Malinyi anaweza kutazama mshahara wake kupitia SimBanking bila kusafiri umbali mrefu kwenda tawini; na mama mjasiriamali wa Mwanjelwa anaweza kupata mtaji kupitia program ya IMBEJU bila dhamana yeyote. Hizi ndizo simulizi za Mission Possible,” aliongeza Raballa akionyesha Benki ya CRDB ilikuwa ya kwanza katika kubuni huduma zote hizo kurahisisha huduma kwa wateja.
“Mfumo huu umeongeza kasi, usalama na ubunifu wa huduma zetu, ukiwezesha matumizi ya akili mnemba na kujihudumia kwa wateja Pia, umefungua fursa ya kupanua huduma zetu katika masoko mapya kama Dubai,” alisema.
Kwa upande wake, Mkuu wa Idara ya Huduma kwa Wateja, Yolanda Uriyo, alisema CRDB Bank inaamini kuwa huduma bora kwa wateja si jambo la msimu bali ni dhamira ya kila siku. “Wiki hii ni fursa ya kuwasherehekea wateja wetu ambao wametupa imani na maoni yanayotuongoza kuboresha huduma kila siku. Pia ni wakati wa kuwapongeza wafanyakazi wetu wanaoishi falsafa ya huduma bora kwa weledi na ubunifu,” alisema.
Akizungumza kwa niaba ya wateja, Hashim Lema aliyekuwa mgeni maalum wa hafla hiyo alitoa pongezi kwa Benki ya CRDB kwa huduma zenye ubunifu, mageuzi ya kidijitali, na ushirikiano wa karibu na wateja wake.