Dar es Salaam, Oktoba 2025: Kampuni ya TotalEnergies Marketing Tanzania imezindua rasmi Kituo chake kipya cha Huduma kilichopo Kimara, jijini Dar es Salaam, ikiwa ni kituo cha kwanza cha kampuni hiyo katika eneo hilo. Uzinduzi huo unalenga kuwakaribia zaidi wateja kwa kuwapatia mafuta ya ubora wa juu na huduma za kuaminika.
Uzinduzi huo umefanyika sambamba na maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja Afrika 2025, ambayo mwaka huu inabeba kaulimbiu isemayo: “Imani Yako, Nguvu Yetu Kila Siku.”
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa TotalEnergies Marketing Tanzania, Mamadou Ngom, amesema uzinduzi wa kituo hicho ni sehemu ya dhamira ya kampuni hiyo ya kuendelea kupeleka huduma za nishati karibu na wananchi.
“Tunapozindua rasmi Kituo cha Huduma cha Kimara, tunaanza pia maadhimisho ya Wiki ya Huduma kwa Wateja Afrika. Hii ni wiki maalum ya kuthamini wateja wetu na kuimarisha uhusiano wa kuaminiana kati yetu. Mafanikio ya TotalEnergies yanatokana na imani ambayo wateja wetu wanaendelea kutuonyesha kila siku,” amesema Ngom.
Kituo kipya cha Kimara kitatoa huduma mbalimbali ikiwemo mafuta ya Excellium, huduma za kadi za mafuta (Fuel Card Services), mafuta lainishi ya ubora wa juu, pamoja na gesi ya kupikia ya TotalEnergies. Huduma zote hizi ziko chini ya mpango wa Dealer-Owned-Dealer-Operated (DODO), unaowawezesha wamiliki wa vituo kushirikiana na TotalEnergies katika upanuzi wa mtandao wa kampuni hiyo nchini.
Kwa upande wake, mmiliki wa kituo hicho, Godfrey Nyashage, amesema uamuzi wake wa kushirikiana na TotalEnergies umetokana na imani yake kwa chapa hiyo.
“Nilichagua TotalEnergies kwa sababu naamini katika nguvu ya chapa yao na maadili yao ya uaminifu. Tangu mwanzo walinipa ushirikiano mkubwa na kuniwezesha kujenga kituo hiki cha kisasa. Ushirikiano huu si wa kibiashara pekee, bali ni wa kiimani, na leo umezaa matunda kwa kuzindua kituo cha kwanza cha TotalEnergies hapa Kimara,” amesema Nyashage.
Uzinduzi wa Kituo cha Huduma cha TotalEnergies Kimara unaashiria hatua muhimu katika mkakati wa kampuni hiyo wa kuendelea kupanua huduma zake nchini Tanzania. Kupitia ubunifu, ushirikiano wa kuaminika na mtazamo unaomlenga mteja, TotalEnergies inaendelea kutoa suluhisho za kisasa, salama na bora za nishati zinazokidhi mahitaji ya kila siku ya Watanzania.


















