Na Emmanuel Mbatilo, Dar es Salaam
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kimezindua mafunzo maalum kwa wahadhiri wake yatakayowawezesha kutumia mfumo wa utoaji elimu kwa njia ya mtandao, kama sehemu ya kuboresha mbinu za ufundishaji na kuendana na maendeleo ya teknolojia.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mafunzo hayo leo, Oktoba 6, 2025 jijini Dar es Salaam, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. William Anangisye, alisema mpango huo ni uwekezaji wa kimkakati katika mtaji wa kiakili wa chuo na katika maendeleo ya rasilimali watu ya taifa.
Amesema mafunzo hayo yanawalenga wahadhiri na wataalamu wa TEHAMA ili kuwawezesha kutumia teknolojia na mbinu bunifu katika ufundishaji na ujifunzaji.
“Kupitia mafunzo haya, tunawaandaa wahadhiri wetu na wataalamu wa TEHAMA kuwa chachu ya mfumo mpya wa elimu unaokumbatia ubunifu, ushirikishwaji na ufundishaji wa kidijitali,” amesema Prof. Anangisye.
Amefafanua kuwa hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa Mradi wa Elimu ya Juu kwa Mageuzi ya Kiuchumi (HEET) unaolenga kuhakikisha wahitimu wa vyuo vikuu nchini wanakuwa na ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira la karne ya 21.
Prof. Anangisye ameongeza kuwa UDSM imejipanga kutekeleza zaidi ya programu 98 za elimu ya mtandaoni na mchanganyiko (blended learning) katika nyanja za sayansi, teknolojia, biashara, sanaa na binadamu, ili kuhakikisha elimu ya juu inapatikana kwa ubora na ufanisi zaidi.
“Kwa kuwapatia wahadhiri wetu ujuzi wa hali ya juu katika uundaji wa kozi za mtandaoni, utengenezaji wa maudhui ya kidijitali na mbinu za kuhamasisha ushiriki wa wanafunzi, tunajenga msingi imara wa uendelevu wa elimu ya mtandaoni nchini,” amesema.
Ameongeza kuwa mpango huo unaendana na Dira ya Maendeleo ya Taifa 2050 na Ajenda ya Umoja wa Afrika 2063, ukiilenga UDSM kuwa kinara wa mageuzi ya elimu ya juu ya kidijitali barani Afrika.
Kwa upande wake, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayeshughulikia Taaluma, Prof. Boniface Rutinwa, amesema UDSM inaendelea kuwekeza katika kuwajengea uwezo wahadhiri wake kutumia mbinu bunifu na shirikishi bila kupoteza ubora wa elimu.
Naye Prof. Benadeta Killian, Naibu Makamu Mkuu wa Chuo anayehusika na Mipango, Fedha na Utawala, ambaye pia ni Mratibu wa Mradi wa HEET, amesema mageuzi hayo ya kidijitali ni sehemu ya juhudi za kuoanisha elimu ya juu na vipaumbele vya kiuchumi vya taifa.
Kwa upande wake, Naibu Mratibu wa Mradi wa HEET UDSM, Dkt. Liberato Haule, amesema kuanzia mwaka wa masomo wa Novemba 2025, UDSM itaanza rasmi kutumia mbinu ya kufundisha kwa njia ya mtandaoni kwa kozi takribani 98 zinazojikita katika fani za Uhandisi, Sayansi, Teknolojia, Biashara, Elimu, Sanaa na Lugha.
“Mbinu hiyo itawapa fursa wengi waliokuwa na ndoto ya kusoma UDSM kupata elimu bila kulazimika kufika chuoni, kwani wataweza kujifunza kwa njia ya mtandao au ana kwa ana,” amesema Dk. Haule.
Naye Mkuu wa Kituo cha Mafunzo ya Mtandaoni (Centre for Virtual Learning – CVL) cha UDSM, Dkt. Fatuma Simba, amesema mfumo huo utasaidia kufikia wanafunzi walioko katika mikoa mbalimbali na hata nje ya nchi bila kuathiri ubora wa elimu.
“Changamoto kubwa imekuwa ni miundombinu isiyotosheleza kuwapokea wanafunzi wote, lakini kupitia teknolojia ya TEHAMA tutawafikia wengi zaidi popote walipo,” amesema Dkt. Simba.
Ameongeza kuwa mfumo huo utasaidia UDSM kuendelea kutoa elimu hata katika nyakati za majanga, akitolea mfano kipindi cha janga la UVIKO-19 ambapo vyuo vililazimika kufungwa.


























