Na. Jacob Kasiri – Misenyi.
Kundi lingine la tembo takribani 50 limeondolewa na Makamanda wa Shirika la Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) kutoka maeneo yaliyokuwa karibu na makazi ya wananchi sanjari na mashamba ya mwekezaji wa kiwanda cha sukari cha Kagera Sugar jana Oktoba 05, 2025 kuelekea Burigi – Chato.
Tembo hao waliswagwa na kuvushwa barabara kuu ya lami inayotokea wilaya ya Misenyi kupitia wilaya ya Karagwe kuelekea Bukoba wakielekezwa kwenda Hifadhi ya Taifa Burigi–Chato, zoezi hilo la kuwavusha lami tembo hao halikuwa rahisi baada ya kuona magari yakipishana katika barabara hiyo.
Hatua hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa maagizo ya Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii, ambayo imezielekeza taasisi zake za uhifadhi kuhakikisha migongano ya muda mrefu kati ya binadamu na wanyamapori hatari na waharibifu inapunguzwa au kuondolewa kabisa.
Kwa mujibu wa maelezo ya TANAPA yaliyodadavuliwa na mratibu wa zoezi hilo Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi Dkt. Fredrick Mofulu Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Ibanda – Kyerwa alisema kuwa lengo kuu ni kulinda usalama wa wananchi, mali zao pamoja na kuimarisha uhifadhi endelevu wa wanyamapori, huku ikiimarisha ushirikiano kati ya jamii na mamlaka za hifadhi.
Aidha, zoezi hilo la kuwaswaga tembo hao takribani 50 kuelekea Burigi – Chato linaendelea leo Oktoba 06, 2025 sambamba na kusakanya makundi mengine yaliyosalia ili kuhakikisha hakuna tembo wanaobaki katika maeneo hayo ya wananchi.