
Utawala wa Rais Donald Trump nchini Marekani unajiandaa kuweka kiwango kipya cha kupokea wakimbizi kuwa watu 7,500 pekee kwa mwaka huu hatua inayopunguza kwa kiasi kikubwa idadi ya wakimbizi ikilinganishwa na 125,000 waliopokelewa mwaka jana chini ya Rais wa zamani Joe Biden.
Kwa mujibu wa duru tatu zilizo karibu na suala hilo, mpango huo mpya unalenga kuwapa kipaumbele wakimbizi weupe kutoka Afrika Kusini, kundi dogo la watu wanaodaiwa kukabiliwa na ubaguzi wa rangi na matukio ya ghasia katika taifa hilo la kusini mwa Afrika.
Hata hivyo, serikali ya Afrika Kusini imekanusha vikali madai hayo, ikisisitiza kwamba hakuna kampeni ya ubaguzi dhidi ya wananchi wake weupe, na kwamba hatua ya Marekani inachochea taswira potofu kuhusu hali halisi ya nchi hiyo.
Taarifa za shirika la habari la Reuters zinaonyesha kuwa kundi la kwanza la wakimbizi 59 kutoka Afrika Kusini lilifika Marekani mwezi Mei, na kufikia 138 mwanzoni mwa Septemba 2025.
Hatua hii inarejelea sera kali za uhamiaji za Trump zilizotekelezwa kati ya mwaka 2017 hadi 2021, wakati alipokuwa akipunguza idadi ya wahamiaji na wakimbizi kama sehemu ya kampeni yake ya “America First.”
Katika Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa uliofanyika wiki iliyopita, Rais Trump alihimiza mataifa mengine duniani kuimarisha ulinzi wa mipaka na kurekebisha mfumo wa kimataifa wa uhamiaji, akisema dunia inahitaji “mfumo mpya unaolinda maslahi ya mataifa.”
Wachambuzi wa siasa za kimataifa wanasema hatua hii ya Marekani inaweza kuibua mvutano wa kidiplomasia na mjadala wa maadili kuhusu namna sera za uhamiaji zinavyotumiwa kama nyenzo ya kisiasa na kijamii.