Na Mwamvua Mwinyi Mafia, Oktoba 7, 2025
WILAYA ya Mafia, mkoani Pwani, imesisitiza ushindani huru katika soko la mwani ili kumnufaisha mkulima, kuinua pato pamoja na kukuza uchumi wa wilaya hiyo .
Kwa mujibu wa takwimu za mwaka wa fedha 2024/2025, mavuno ya mwani yalifikia tani 600 zenye thamani ya sh.milioni 420, kwa bei ya wastani ya Sh.700 kwa kilo.
Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Aziza Mangosongo, anasema serikali inaruhusu ushindani wazi wa wanunuzi wa mwani kwa kuzingatia sheria na miongozo iliyopo, bila kuwepo kwa ukiritimba , ama mnunuzi mmoja au kampuni.
Mangosongo aliyasema hayo Oktoba 6, 2025, katika kikao kilichowakutanisha wadau wa kilimo cha mwani wilayani humo, kilicholenga kujadili na kutafuta suluhisho kwa baadhi ya changamoto zinazowakabili wakulima hao ikiwemo uwepo wa mnunuzi mmoja mkubwa, kampuni ya Mwani Mariculture, anayehodhi soko kwa sasa.
“Sisi kama Mafia tunaenda na azimio la kufungua milango kwa wanunuzi wengine kuingia sokoni, tunataka taratibu zifuatwe na kila kitu kinachowahusu wakulima kipitie halmashauri ili Idara ya Kilimo iwe na taarifa sahihi,” alielezea Mangosongo.
Aidha, alibainisha kuwa lengo ni kuhakikisha wakulima wananufaika moja kwa moja, huku bei ya mwani ikitarajiwa kupanda kutoka Sh.800 hadi kufikia Sh.1,000 kwa kilo.
Vilevile Mkuu huyo wa wilaya aliagiza wataalamu wa kilimo, kupata takwimu sahihi kuhusu wakulima waliopo na hali halisi ya zao hilo ili kuwezesha kuweka mikakati ya kiutekelezaji inayoendana na uhalisia wa kilimo cha mwani kisiwani humo.
Rabihu Hemedi, mkulima wa mwani kutoka kijiji cha Banja, alieleza kuwa changamoto kubwa wanayokabiliana nayo ni ukosefu wa vitendea kazi na ujuzi wa kisasa wa kilimo hicho.
Anasisitiza ,elimu kwa wakulima ni muhimu ili kuongeza thamani ya zao hilo, kukuza soko, na kuwezesha uanzishwaji wa ushirika wa wakulima.
“Zao la mwani limetusaidia hasa kina mama walikuwa hawana shughuli ya kufanya zaidi ya uvuvi, sasa wanapata kipato na limepunguza shinikizo kwenye uvunaji wa samaki na mazao mengine ya baharini,” alieleza Rabihu.
Kwa upande wake, Nasri Basha, mkulima kutoka Kiegeani, aliishukuru Serikali ya Wilaya kwa hatua ya kufungua soko na kuomba iendelee kupeleka wataalamu kwa wakulima ili waweze kujifunza mbinu za kilimo cha kisasa cha mwani na kusaidia mchakato wa kuanzisha ushirika rasmi.
Kwa mujibu wa Basha, mafanikio ya kilimo cha mwani na uvuvi kwa ujumla yanachangiwa kwa kiasi kikubwa na uhifadhi wa mazingira unaoendelezwa na mashirika na taasisi mbalimbali ikiwemo Hifadhi ya Bahari Mafia (HIBAMA), Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) na jamii
Ofisa Uvuvi wa Wilaya, Alfahad Mohamed, alisema kuwa asilimia 90 ya wakulima wa mwani ni wanawake, na kilimo hicho kimekuwa chanzo kikuu cha ajira na kipato kwao.
“Licha ya kuuza mwani ghafi, tunaendelea kuhamasisha uongezaji wa thamani ili wakulima watengeneze bidhaa mbalimbali kama sabuni, mafuta, na virutubisho kutokana na mwani,” alieleza Alfahad.
Naye Albert Makalla, Mhifadhi Shirikishi kutoka HIBAMA, alisema taasisi hiyo inaendelea kutoa mafunzo kupitia wataalamu kutoka ndani na nje ya nchi, kwa lengo la kuwawezesha wakulima kuongeza ubora na thamani ya mwani.
“Tunatoa wito kwa wakulima kuchangamkia fursa za mafunzo mara zinapotolewa, ili kuimarisha uzalishaji na ushindani wa mwani wa Mafia katika soko la kitaifa na kimataifa,” alihimiza Makalla.