Na Said Mwishehe,Michuzi TV-Mwanza
MGOMBEA urais kupitia Chama Cha Mapinduzi(CCM) Rais Dk.Samia Suluhu Hassan ametoa rai kwa Watanzania kuliheshimisha Taifa ndani ya nchi na nje ya nchi huku pia akisisitiza kuiheshimisha nchi yetu kwa kuweka amani, kufanya chaguzi bila matatizo, bila vurugu.
Pia kuheshimisha nchi yetu kwa kufuata sheria zilizopo nchini, kufuata haki na kila mtu anapata haki yake na mambo kama hayo ndani ya nchi lakini nje ya nchi ni kuimarisha uhusiano kidiplomasia ambao mpaka hatua tuliyofikia jina letu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni zuri sana linaheshimika.
Akizungumza katika mkutano wa hadhara uliofanyika Uwanja wa Tabasamu wilayani Sengerema mkoani Mwanza Mgombea urais Dk.Samia pamoja na kuzungumzia maendeleo yaliyopatikana miaka mitano iliyopita katika mkoa huo amezungumzia kuhusu umuhimu wa kuliheshimisha jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
“Ni wajibu wetu kuheshimisha Taifa ndani ya nchi na nje ya nchi, tutaheshimisha nchi yetu kwa kuweka amani kifanya chaguzi bila matatizo, bila vurugu lakini kuheshimisha nchi yetu kama tunafuata sheria zetu, tunafuata haki kwa kila mtu anapata haki yake na mambo kama hayo ndani ya nchi.
“Lakini nje ya nchi ni kuimarisha uhusiano kidiplomasia ambao mpaka hatua tuliyofikia jina letu Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni zuri sana linaheshimika. Hayo ndiyo mambo ambayo nchi yetu serikali yenu mkitupa ridhaa tunakwenda kuendeleza mambo yote yanayolenga mahusiano ya kijamii.”
Akifafanua zaidi amesema “Wapo Watanzania ambao kila wakiona jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania linaheshimika duniani kazi yao ni kushusha heshima ya nchi yao. Nawaomba tuachane nao, waacheni waende kivyaovyao. Hao siyo wenzetu.”
Katika hatua nyingine, Dk.Samia amewapongeza wana Sengerema ambao wanakwenda kuzindua mgodi mkubwa wa Nyansaka ambao ni mkubwa kuliko yote nchini Tanzania ambao utatoa ajira nyingi kwa vijana lakini pia utatoa fursa za biashara nyingi kwa wafanyabiashara kwa mkoa huu wa Mwanza.
Kuhusu uchaguzi mkuu mgombea urais Dk.Samia amesema Chama Cha Mapinduzi(CCM) inaomba Watanzania tarehe 29 waichague ili wakafanye hiyo kazi ya kuleta maendeleo kama ambavyo imeelezwa ndani ya Ilani na hiyo ni kwa Tanzania nzima.
“Nataka kuwaambia tumeweza na tutaweza, tunajiamini, tutaweza kuyatekeleza yaliyomo kwa hivyo basi mimi mgombea urais, wabunge na madiwani.
“Tunawaomba tutoke wote twendeni kwa pamoja amsha rafiki yako, familia, kila aliyeandikishwa ndani ya nyumba yako toka naye, mabalozi wetu hakikisheni watu wako wote waliondikishwa wanakwenda kupiga kura.
“Nendeni kachagueni chama cha mapinduzi Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania wa chama cha mapinduzi. Wabunge wa Chama Cha Mqpinduzi.
“Madiwani ambao wanasimamia utekelezaji wa miradi kwenye maeneo yenu kachagueni wa ccm mkiwachanganyia sauti zitagongana. Huyu anasema ndiyo huyu anasema siyo.Huyu anasema tukajenge huyu anasema subiri.”