

Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) limetoa wito kwa Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina na wa haraka kuhusu taarifa za kutekwa kwa aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Humphrey Polepole.
Wito huo umetolewa leo, Oktoba 7, 2025, na Mwenyekiti wa TEF, Deodatus Balile, kupitia taarifa kwa vyombo vya habari, ambapo alisisitiza umuhimu wa kulinda amani na haki za binadamu nchini.
“Tunaamini kama ni siasa, basi wafuasi na viongozi wa vyama vya siasa wanapaswa kupewa mafunzo ya kushiriki siasa zenye lengo la kuleta maisha bora kwa Watanzania, kwa kushindanisha hoja — si kuviziana, kuangushana au kutekana. Kwa kauli moja tunasema, utekaji haukubaliki Tanzania,” imeeleza taarifa hiyo.
TEF imesisitiza kuwa kutokana na sifa ya muda mrefu ya Tanzania kama nchi ya amani, si vyema kuona taswira hiyo ikipotea kutokana na matukio ya usalama yanayoibuka sasa.
“Kwa vyovyote iwavyo, sisi kama Jukwaa la Wahariri Tanzania tunasema, maisha na uhai wa Watanzania ni kipaumbele namba moja kwa amani ya Taifa letu — na amani ni tunda la haki,” taarifa hiyo imeongeza.
Aidha, TEF imekiri kufuatilia kwa karibu taarifa za kutekwa kwa Balozi huyo mstaafu, ikikumbusha kuwa jamii bado haijasahau matukio ya utekaji na mauaji ya watu mbalimbali nchini yaliyowahi kuripotiwa miaka ya nyuma.









