Madaktari bingwa wa upasuji wa moyo na mishipa ya damu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) na wenzao kutoka Shirika la Cardio Start International la nchini Marekani wakimfanyia upasuaji wa kupandikiza mishipa ya damu mgonjwa ambaye mishipa yake ya damu imeziba wakati wa kambi maalumu ya siku tano inayofanyika katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es Salaam.
Daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kutoka Shirika la Cardio Start International la nchini Marekani Richard Harper akiwafundisha wataalamu wa afya kutoka hospitali mbalimbali nchini namna ya kumuhudumia mgonjwa wa dharura wakati wa mafunzo ya kuhudumia wagonjwa wa dharura na mahututi yanafanyika kwa siku nne katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) iliyopo jijini Dar es Salaam. (Picha na JKCI).
…………
Na Mwandishi Maalumu-Dar es Salaam.
Wagonjwa 15 wenye matatizo ya mishipa ya damu ya kifua kutanuka au kuchanika (Ascending Aortic Aneurysm and Dissection) wanatarajia kufanyiwa upasuaji wa moyo na watalaamu wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na wenzao kutoka Shirika la Cardio Start International la nchini Marekani.
Upasuaji huo unafanyika katika kambi maalumu ya siku tano inayofanyika katika Taasisi hiyo iliyopo jijini Dar es salaam.
Akizungumza na mwandishi wa habari hii daktari bingwa wa upasuaji wa moyo na mishipa ya damu kutoka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Alex Benjamini alisema wataalamu wa Cardio Start International walianza na kutoa mafunzo ya kuwajengea uwezo ambayo yatatusaidia kuendelea kutoa huduma bora kwa wagonjwa wao.
“Katika kambi hii tutawafanyia upasuaji wagonjwa wenye matatizo ya mishipa ya damu mikubwa kutanuka au kuchanika, tutazibua mishipa ya moyo iliyoziba na kuziba milango ya moyo inayovuja”, alisema Dkt. Alex.
Dkt. Alex alisema kambi hiyo inatoa fursa kwa wagonjwa wenye matatizo ya mishipa ya damu kupata huduma bingwa bobezi za matibabu ya moyo na kuboresha afya zao.
Kwa upande wake Daktari kutoka Shirika la Cardio Start International la nchini Marekani Mark Napoli alisema Cardio Start International imekuwa ikishirikiana na JKCI katika kutoa huduma za kibingwa wakiwa na lengo la kubadilishana ujuzi na uzoefu.
“Hii ni mara yangu ya pili kufanya kazi na wataalamu wa JKCI, wana ujuzi na vifaa vya kisasa hivyo kutupa wakati mzuri wakupeana mbinu mpya katika kutoa huduma za matibabu ya moyo na mishipa ya damu”, alisema Dkt. Mark.
Dkt. Mark alisema mbali na kufanya upasuaji wa moyo na mishipa ya damu wataalamu hao pia wanatoa mafunzo kwa wataalamu kutoka hospitali mbalimbali nchini ili kwa pamoja waweze kuwatambua na kuwasaidia wagonjwa wa moyo.