
Katibu Mkuu mstaafu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dk. Bashiru Ally, amesema hana wasiwasi na mustakabali wa nchi, akibainisha kuwa Watanzania hawawezi kuivunja nchi yao kama baadhi ya kauli za vijana zinavyodai.
Akizungumza leo, Oktoba 8, 2025, katika mkutano wa kampeni za CCM uliofanyika Uwanja wa Nyamagana, jijini Mwanza, Dk. Bashiru amesema Watanzania ni watu wa amani, waliokomaa kisiasa na wanaoelewa umuhimu wa umoja wa kitaifa.
“Nasikia maneno kutoka kwa vijana kana kwamba kuna wasiwasi hivi. Nawahakikishia kuwa huyu kiongozi wetu anayeomba ridhaa tena, amepitia majaribu, ameshajaribiwa na ameshinda majaribu. Tuna uhakika tutavuka salama,” amesema Dk. Bashiru.
Ameongeza kuwa Tanzania imeendelea kubaki imara licha ya kupitia kipindi kigumu cha mabadiliko ya ghafla ya uongozi wa nchi, jambo linaloonyesha uthabiti wa chama na Serikali.
“Kama nchi imebaki nchi moja, chama kimeendelea kuwa kimoja, na usalama umetamalaki katika kipindi kigumu cha mabadiliko ya serikali ya ghafla, basi hizi ramsharamsha na vijimaneno vya kupanga ni rahisi kuvidhibiti,” ameongeza.
Aidha, Dk. Bashiru amesisitiza kuwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan ameandaa vizuri chama na nchi kuelekea uchaguzi mkuu ujao, jambo linalodhihirishwa na utulivu unaoonekana katika mikutano yake ya kampeni.
“Dk. Samia amekiandaa chama na nchi kushiriki uchaguzi mkuu, ndiyo maana wananchi wanatulia katika mikutano yake wakimsikiliza kwa makini,” amesema.